Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MADAKTARI BINGWA WA RAIS SAMIA WATOA MAFUNZO YA MASHINE YA 'CPAP' HOSPITALI YA MANGAKA

Posted on: September 19th, 2025

Na Waf, Mtwara

Timu ya Madaktari Bingwa wa Rais Samia imetoa mafunzo ya matumizi ya mashine kusaidia watoto wachanga wenye shida ya upumuaji (CPAP) katika hospitali ya Wilaya ya Mangaka.

Hayo yamebainishwa leo 18 Septemba, 2025 na Muuguzi Bingwa wa Huduma za Ukunga na Afya ya Uzazi Bw. Stanuel Kosani katika kambi ya madaktari bingwa wa Rais Samia inayoendelea katika hospitali ya Wilaya ya Mangaka mkoani Mtwara.

Bw. Kosani amesema Katika wodi ya watoto wachanga kuna vifaa tiba vya kutosha ikiwemo mashine ya CPAP ambayo ni nzuri kwa ajili ya kusaidia watoto wachanga wenye shida ya upumuaji na inauwezo wa kupunguza vifo vya watoto wachanga kwa kiasi kikubwa.

"Mara baada ya kufika na kukuta mashine hizo zipo tumekaa nao na tume elekezana namna ya kuzipanga na kuzitumia na kuanza kutumika mara moja kwa watoto waliokuwa na shida ya upumuaji," amesema Dkt. Kosani.

Pia ameishukuru Serikali kwa kuwawezesha kufika hospitalini hapo kwani wanavyoendelea kufika mara nyingi zaidi watumishi wanapata ujuzi wa kutosha na itasaidia sana kuokoa vifo vya watoto wachanga.

Naye Muuguzi Kiongozi wa Wodi ya Wazazi katika hospitali hiyo Bi. Zubeda Namangaya amesema madaktari hao mbali na kutibu pia wamefanya kazi kubwa ya kujengea uwezo watumishi waliopo juu ya kutumia mashine mbalimbali za kisasa katika kuhudumia watoto wachanga.

"Kitengo cha watoto wachanga tulikuwa na mashine ya CPAP tulikuwa hatuna uwezo wa kuitumia ila kwa sasa tumejengewa uwezo wa kuitumia kusaidia watoto wachanga pia namna ya kutumia mashine ya incubator na phototherapy," amesema Bi. Namangaya

Pia amesema ujio wa madaktari hao umekuwa na tija kubwa kwani ujuzi waliojengewa utawafanya kujiamini kazini na kufanya kazi ya kuokoa mama na watoto katika hospitali hiyo kwa gharama nafuu na bila rufaa ya kwenda mbali na maeneo wanayoishi.