MADAKTARI BINGWA WA RAIS SAMIA WATOA MAFUNZO ELEKEZI KYELA
Posted on: October 5th, 2024Na WAF - MBEYA
Timu ya Madaktari Bingwa na Bobezi ya Rais Samia imeendesha mafunzo elekezi kwa watoa huduma za afya katika Hospitali ya Wilaya ya Kyela, mkoani Mbeya, kwa shabaha yakuwaajengea uwezo watoa huduma wa Halmashauri hiyo.
Mafunzo haya yamefanyika Oktoba 04, 2024, na kuongozwa na Dkt. Halima Mohamed Abass, Daktari Bingwa wa Watoto, shabaha ikiwa nikuwafanya wataalam hao kuongeza ufanisi wa watoa huduma.
“Mafunzo haya ni sehemu ya mikakati ya serikali ya kuboresha huduma za afya kwa wananchi na kuhakikisha kila kituo cha afya kina wataalamu waliobobea na kuwa na weledi stahili kwenye utoaji huduma,” ameeleza Dkt. Halima na kuongeza
“Ni muhimu kila mhudumu wa afya anakuwa na ujuzi wa kisasa ili kuboresha matokeo ya afya kwa wagonjwa wetu, hususan watoto ambao wanahitaji uangalizi wa kipekee kwani Serikali chini yauongozi imara wa Rais Samia Suluhu Hassan imewekeza vyakutosha katika miundombinu na vifaa tiba vya kisasa,” amesisitiza Dkt. Halima
Tunafanya kazi kwa karibu kuhakikisha kila kituo cha afya kina wataalamu waliobobea na wenye mafunzo ya kutosha ili kuboresha afya ya wananchi kwa ujumla,” amesema Dkt. Halima.
Pia, Dkt. Halima amebainisha umuhimu wa watoa huduma kujua kutumia vifaa tiba kwa usahihi, kwani vifaa hivi vina uwezo mkubwa wa kuboresha matibabu endapo vitatumika ipasavyo na kusaidia wananchi wa maeneo hayo.
“Mafunzo haya yatawawezesha kujifunza mbinu bora za kutumia teknolojia na vifaa vya kisasa ili kutoa huduma bora zaidi kwa wagonjwa na kupunguza rufaa zisizoza lazima” ameongeza.
Dkt. Halima amewahimiza wananchi wa Kyela kuchangamkia fursa hii ya kipekee ya kupata huduma za kibingwa, akiwataka wajitokeze kwa wingi ili wapate vipimo, ushauri, na matibabu kutoka kwa madaktari waliopo kwa ajili yao.