MADAKTARI BINGWA WA RAIS SAMIA WAHIMIZWA KUWAJENGEA UWEZO WATUMISHI MAHALA PA KAZI
Posted on: October 16th, 2024
Na WAF - Pwani
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Aboubakar Kunenge amewasihi Madaktari Bingwa ambao wameweka kambi ya kutoa matibabu mkoani humo kuhakikisha ujuzi na uwezo wa kibingwa walionao wana wapa na wataalamu waliopo vituoni hapo.
Mhe. Kunenge ameyasema hayo leo Tarehe 15 Oktoba, 2024 alipo kutana na baadhi ya Madaktari Bingwa hao kujua mwenendo wa utoaji wa huduma katika kambi hizo.
"Kitu kikubwa ninacho waomba ni kuwapa mafunzo katika vituo mnavyo enda kutoa huduma kuhakikisha utaalam mlio nao mnaweza kuwapatia watumishi waliopo kwani hospitali zetu zina vifaa tiba vya kutosha na vya kisasa," amesema Dkt. Kunenge.
Pia Mhe. Kunenge amewashukuru madaktari hao kwa kujitoa kwa moyo wote kuweza kuhakikisha huduma zote wanazo toa katika hospitali zao wanaweza kuwapatia wananchi katika ngazi ya afya ya msingi kwa gharama ile ile.
"Ni imani yangu kwa hiki mnachokifanya ni ibada kwa kuokoa maisha ya watu, ukiokoa maisha ya mtu ni ibada kwako pia na mungu anakubariki," amesema Mhe. Kunenge
Nae Daktari Bingwa wa Usingizi na Ganzi Salama Dkt. Edwin Luganzia kwa niaba ya Madaktari Bingwa hao amesema watahakikisha wanafanya kazi sambamba na watoa huduma waliopo ili kuweza kuwajengea uwezo wa kutoa huduma za afya za kibingwa.
"Tutafanya kazi na watoa huduma waliopo kwa vitendo kubadilishana mawazo na uzoefu na vilevile kuhakikisha tunaboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya," amesema Dkt. Luganzia