Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MADAKTARI BINGWA WA RAIS SAMIA WAFIKISHA HUDUMA RUNGWE

Posted on: September 18th, 2025

Na WAF, RUNGWE

Serikali kupitia na Wizara ya afya imeendelea kuratibu utoaji wa huduma za wa Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia kwa kuwapatia huduma za matibabu ya kibingwa wananchi wa mji wa Tukuyu katika hospitali ya Halmashauri ya Tukuyu wilayani Rungwe mkoa Mbeya.

Akizungumza leo Septemba 17, 2025, mzazi wa mtoto aliyefanyiwa upasuaji wa uvimbe uliokuwa karibu na jicho, Bi. Rose Kaswese
amesema, amefurahishwa na ujio wa Madaktari hao kwasababu imemrahisishia mtoto wake kupata matibabu na kufanyiwa upasuaji haraka pia ameipongeza Serikali kwa kuwasogezea huduma za kibingwa karibu na maneno yao.

“Mtoto wangu alipata uvimbe karibu na jicho akiwa na miezi mitatu, nimehangaika kutibiwa hospitali nyingi lakini ilishindikana na uvimbe ulizidi kukua, lakini nilivyosikia tangazo la ujio wa Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia ikanilazimu kufika na mwanangu ameshapatiwa matibabu, Tunaishukuru Serikali,” amesema Bi. Kaswese.

Naye Bi Elukaga Lwitiko amesema ujio wa Madaktari Bingwa na bobezi wa Rais Dkt. Samia unachochea utoaji wa huduma bora kwa wagonjwa lakini pia imeleta unafuu katika kupunguza gharama zisizo za msingi.

“Kwakweli Ujio wa Madaktari Bingwa tumeufurahia, inatupunguzia gharama ya kwenda Muhimbili, tunaomba suala hili liwe endelevu ili tuzidi kupata msaada” amesema Bi. Lwitiko.

Kwa upande wake Mganga
Mfawidhi wa Hospitali ya Tukuyu, Dkt. Emmanuel Asukile amesema Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia wamehudumia wagonjwa wengi wakiwemo watoto, wazee, wajawazito, wenye uvimbe, na wagonjwa wa Upasuaji.

Aidha Dkt. Asukile amesema kupitia ujio huo wanapata ujuzi wa kutumia vifaa mbalimbali vya matibabu.