Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MADAKTARI BINGWA WA RAIS SAMIA NA MANUFAA NGAZI YA MSINGI

Posted on: September 28th, 2024

Na WAF, Manyara

Uwepo wa madaktari bingwa kupitia mpango wa Rais Samia Suluhu Hassan umeleta manufaa makubwa kwa wanachi baada ya kufikisha huduma za kibingwa na Bingwa Bobezi hadi ngazi ya halmashauri.

Akizungumza Septemba 28, 2024 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Bw. Ismail Rumatila amesema wananchi zaidi ya 69,797 wamepatiwa matibabu katika awamu ya kwanza ya kambi hizo, hatua inayoonyesha jinsi zilivyo na manufaa.

Amesema idadi hiyo ya wananchi imeonesha muitikio mkubwa wa wananchi jambo linaloonesha wazi huduma zilikua hitajio kwa watu walio wengi hali iliyochagia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI kuja na mpango awamu ya pili.

“Baada ya kuhitimisha zoezi la awali, Wananchi na wadau mbalimbali waliomba huduma hizi ziwe zinafanyika kila mara ambapo Serikali ilisikia ombi hilo na kuiagiza Wizara ya Afya na OR TAMISEMI kulitekeleza”. Amesema Bw. Rumatila

Pia, Bw. Rumatila ameeleza kuwa hadi kufikia leo madaktari bingwa hao wamefanikiwa kuwahudumia jumla ya wananchi 3,287 ambapo waliotibiwa na kuondoka 2,895, waliolazwa 173, waliofanyiwa upasuaji ni 85 na waliopewa rufaa ni 134.

Ameongeza kuwa madaktari bingwa hao wameweza kufanikisha kufufua na kuanzisha matumizi ya vifaa tiba vilivyokua havitumiki katika hospitali hizo, pamoja na kuwajengea uwezo watumishi wa afya jinsi ya kutumia vifaa hivyo.

“kupitia kambi hii mambo muhimu wameweza kuanzisha kama vile mashine ya usingizi na ganzi kwa ajili ya huduma endelevu katika hospitali walizokaa ikiwemo pamoja na kuwajengea uwezo wataalam wetu waliopo katika hospitali za Halmashauri.” Amesema Bw. Rumatila