Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MADAKTARI BINGWA WA RAIS SAMIA KUHUDUMIA WAKAZI WA PWANI KWA SIKU SABA

Posted on: October 15th, 2024

Na WAF Pwani

Madaktari Bingwa 55 wa fani mbalimbali wanatarajia kutoa huduma za matibabu ya kibingwa na bobezi kwa siku saba katika Halmashauri tisa (9) za mkoa wa Pwani.

Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani Dkt. Kusirye Ukio wakati wa hafla ya kuwapokea Madaktari Bingwa ambao watatoa huduma kuanzia tarehe 14 hadi 20 Oktoba, 2024

Dkt. Ukio amesema mkoa wa Pwani umepokea Madaktari Bingwa 55 kutoka nyanja za huduma ya afya ya uzazi mama na mtoto, afya ya kinywa na meno, usingizi na ganzi salama, upasuaji, mifupa na wakunga wabobezi wa nyanja mbalimbali ambao watasambazwa kutoa huduma katika mkoa wa Pwani kwa muda wa siku tano (5)

"Tumepokea kwa mikono miwili zoezi hili ambalo ni la ki ibada kwa watumishi hawa ambao wametenga muda wao kwa ajili ya kuwahudumia wananchi katika maeneo ambayo siyo rahisi kufikika ama wao kufikia huduma za kibingwa kama watakazozipata," amesema Dkt. Ukio.

Dkt. Ukio amesema maandalizi mazuri yamefanyika kwa kuhamasisha jamii na kuwatayarisha watoa huduma wa vituoni ili kushirikiana na madaktari hao na kupata ujuzi.

Pia Dkt. Ukio amewaomba wananchi wa mkoa wa Pwani kutumia fursa hiyo kujitokeza kwa wingi katika hospitali za Halmashauri, ili kupata huduma za kibingwa kutoka kwa madaktari hao.

Kwa upande wake Mratibu kutoka Wizara ya Afya Bw. Michael Mbele amesema lengo kubwa la kampeni hiyo ni kuwawezesha wananchi wasio na uwezo wa kuzifikia huduma za kibingwa katika hospitali kubwa, kupata huduma hizo katika maeneo yao.