MADAKTARI BINGWA CHACHU YA UBORESHAJI HUDUMA NGAZI YA MSINGI
Posted on: September 24th, 2025
Na WAF -Mji Mwema, Songea.
Kambi ya Madaktari Bingwa iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwenye kituo cha afya Mji Mwema ni ishara ya mafanikio na manufaa makubwa kwa wananchi na fursa ya kuboresha mfumo wa utoaji huduma za afya kwa ngazi ya msingi.
Hali hiyo imebainishwa leo Septemba 23, 2025 na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Afya ya Uzazi Dkt. Joshua Kileo kuwa kumekuwa na muitikio wa wananchi wengi na wametambua hiyo ni fursa itakayowapunguzia safari ya kufuata huduma za kibingwa.
“Wanawake wengi wamejitokeza kupata huduma juu ya changamoto za uzazi na tumbo lakini pia kupata elimu na ushauri juu ya masuala mazima ya uzazi, “ Amesema Dkt. Kileo.
Dkt. Kileo amesema programu ya madaktari bingwa wa mama Samia imewezesha kugundua changamoto na jitihada za hospitali na za wauguzi kwani katika kushirikiana kutoa huduma na wahudumu wa Afya ngazi ya msingi wanatoa nafasi kwa vituo vya afya kukua zaidi kihuduma kwa maana ya utendaji kazi lakini pia matumizi ya vifaa maalum vya kutolea huduma za kibingwa.
“Kupitia ujio wa madaktari bingwa wa mama Samia inaleta kukua kwa vituo vya afya kwani ili daktari bingwa aweze kufanya kazi katika kituo cha afya ni lazima kuwepo na upatikanaji wa vifaa vya kutolea huduma za kibingwa.
Naye Muuguzi Mbobezi Bi. Beatrice Pyuza kutoka Hospitali ya Ngarenaro, Arusha amesema programu husika inawapa fursa ya kushirikiana na kutoa huduma bora na kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.
“Mimi kama muuguzi mbobezi tunaposhirikiana na wahudumu wa afya katika kituo cha afya cha Mji Mwema tunatoa huduma bora na kuwajengea uwezo wauguzi ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi lakini pia kutoa elimu kwa wateja juu ya Baba kushiriki kliniki pindi mwenza anapokua mjamzito na baada ya ujauzito.
Madaktari hao pia wamepongeza ushirikiano mkubwa kutoka kwa wananchi, uongozi wa hospitali na Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwa kuwawekea mazingira rafiki ya kufanikisha zoezi hilo.