Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MADAKTARI BINGWA 43 WAWASILI MANYARA KUTOA HUDUMA ZA AFYA BOBEZI

Posted on: October 6th, 2025

Na, WAF. Manyara

Timu ya madaktari bingwa bobezi wa Rais Samia imewasili mkoa wa Manyara na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Cuthbert Sendiga kwa lengo la kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi katika Halmashauri saba (7) kwa muda wa siku sita

Mhe. Sendiga akizungumza mara baada ya kuwapokea madaktari hao leo Oktoba 6, 2025 amesema uwepo wa timu ya madaktari bingwa mkoani humo kunapunguza adha ya wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo katika hospotali za Mikoa, Kanda hadi Hospitali ya Taifa Muhumbili.

Amesema, timu ya madaktari bingwa imekuwa chachu ya kusaidia mabingwa wa ndani ya mkoa kupata ujuzi na kuongeza wigo na ufanisi wa kutoa matibabu kwenye maeneo mbalimbali mkoni humo, hivyo hata baada ya kuondoka mkoa huendeleza huduma hiyo bobezi kwa wananchi.

“Uwepo wenu unasaidia kuongeza maarifa na uwezo wa mabingwa waliopo ndani ya mkoa, kupanua wigo wa huduma na kuongeza ufanisi wa matibabu ili hata mkiondoka huduma hizi ziendelee kutolewa kwa wananchi,” amesema Mhe. Sendiga.

Aidha, Mratibu wa huduma za kibingwa kutoka Wizara ya Afya Bi. Fidea Obimbo amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea kusogeza huduma karibu zaidi kwa wananchi na sasa hii ni awamu nyingine kwa timu hiyo inahusisha madaktari bingwa kuwafikia wananchi wasioweza kuzifuata huduma za kibobezi kwa urahisi kutokana na gharama au umbali.