Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MADAKTARI BINGWA 26 WA RAIS SAMIA WAWEKA KAMBI YA MATIBABU NJOMBE

Posted on: September 22nd, 2025

Timu ya Madaktari, Wauguzi Bingwa na Bobezi wapatao 36 wametua mkoani Njombe kwa ajili ya kutoa huduma za Kibingwa na Ubingwa Bobezi kupitia Program ya Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni awamu ya nne kufanyika katika mkoa huo.

Wataalam hao wamepokelewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe Bi. Judica Omari, pamoja na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dkt. Juma Mfanga, ambao wametawanywa katika Hospitali za Halmashauri sita zinazounda Mkoa huo, wakitarajiwa kutoa huduma za Ubingwa katika maeneo ya magonjwa ya ndani, wanawake na ukunga, upasuaji, ubobezi kwa watoto wachanga, ubingwa katika huduma za kinywa na meno, usingizi na ganzi, pamoja na huduma za ubingwa na ubobezi katika uuguzi.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kambi hiyo Septemba 22, 2025 Katibu Tawala, Bi Judica Omari amewataka wananchi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi, huku akiwataka watumishi wa afya waliopo katika Hospitali hizo kutumia vyema fursa ya kujengewa uwezo katika maeneo yao ya kazi.

Ameongeza, uwepo wa kambi hizo umesaidia kupunguza gharama za matibabu kwa wananchi, kwa kuwafikishia huduma za ubingwa katika maeneo yao, hali inayookoa muda na kupunguza gharama za usafiri kwa mgonjwa na ndugu wanaouguza.

Naye Mratibu wa Kambi ya Madaktari Bingwa na Bingwa Bobezi mkoani Njombe, Bi. Paskalina Andrea, amesema kambi hizo zimekuwa na ufanisi mkubwa katika ustawi wa afya za wananchi, pamoja na maboresho ya huduma mbalimbali, mathalani;- wagonjwa zaidi ya 200,000 wakipatiwa huduma katika awamu ya tatu, huku kati yao zaidi ya 16,000, wakifanyiwa upasuaji.

Ameeleza pia kuwa uwepo wa Kambi hizo umeenda sambamba na maboresho katika vyumba vya kulaza watoto wachanga (NCU), vyumba vya upasuaji, vyumba vya kujifungulia na kuwajengea uwezo watumishi waliopo katika Hospitali hizo.

Kambi za Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkoa wa Njombe zitahitimishwa Septemba 26, 2025 huku jozi ya Madaktari sita (6) kwa kila Hospitali za Halmashauri za Makambako, Wanging’ombe, Makete, Ludewa, Njombe DC na Njombe TC wakienda na kaulimbiu isemayo “ Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia, tumekufika; karibu tukuhudumie.”