MABORESHO YA MPANGO KAZI WA HUDUMA ZA AFYA NGAZI YA JAMII KULETA TIJA
Posted on: September 20th, 2025
Imeelezwa kuwa maboresho ya Mpango kazi wa Huduma za afya Ngazi ya Jamii yataongeza chachu ya ufanyaji kazi kwa weledi na kusaidia jamii kwa ujumla.
Hayo yamebainishwa hivi karibuni na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu kutoka Wizara ya Afya, Bw. Issa Ng’imba, katika ufunguzi kikao kazi kilichowashirikisha viongozi mbalimbali na wadau wa afya jijini Dar es Salaam.
Bw. Ng'imba amesema maboresho hayo yatahakikisha kila mhudumu wa afya ngazi ya jamii anaongozwa na mpango kazi thabiti utakaorahisisha utoaji wa huduma na kuchangia katika kupunguza mzigo wa magonjwa.
"Mpango kazi huu utakapokamilika utakuwa dira ya utekelezaji wa majukumu ya wahudumu wa afya ngazi ya jamii wenye lengo la kupunguza idadi ya wagonjwa wanaofika katika vituo vya kutolea huduma za afya," amefafanua Bw. Ng'imba.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Kinga, Dkt. Otilia Gowelle, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wizara na wadau mbalimbali katika kuboresha mpango kazi huo.
Amewataka wadau wa afya kuendelea kuchangia mawazo na mapendekezo ili mpango kazi wa miaka mitano ujao uweze kutatua changamoto za afya, ustawi wa jamii na lishe zinazokumba jamii.
Kikao kazi hicho kimehudhuriwa na viongozi, wadau mbalimbali wa afya, wakiwemo waratibu wa afya ngazi ya jamii, watendaji wa kata na vitongoji, wahudumu wa afya ngazi ya jamii na wakuu wa vituo vya afya.