MABARAZA YA UDAKTARI , UKUNGA NA UUGUZI KUTUMIA MIFUMO MASUALA YA TAALUMA
Posted on: August 14th, 2024
Na WAF - Dodoma
Mwenyekiti Kamati ya kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI Mhe. Elibariki Kingu (MB) amelitaka Baraza la Madaktari Tanganyika pamoja na Baraza la Uuguzi na Ukunga kutumia mifumo ya kieletroniki ili kupunguza gharama na kuboresha huduma za usimamizi wa mabaraza.
Mhe. Kingu amesema hayo leo Agosti 14, 2024 kwenye kikao cha kamati ya kudumu ya Bunge ya Afya na masuala ya UKIMWI kilichofanyika ukumbi wa Bunge, jijini Dodoma baada ya wasilisho la taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Baraza la Madaktari Tanganyika na Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania.
“Mabaraza haya yanafanya kazi kubwa ya kuhakikisha weledi wa kazi na taaluma unaimarika, asilimia kubwa ya Watanzania wanapata huduma kupitia watumishi wa Sekta ya Afya ambao wanatakiwa kupitia kwenye mabaraza haya, ni muhimu kuweka mifumo yenu ya kielectroniki vizuri ili kupunguza gharama na kuboresha huduma hizi kwa madaktari, wauguzi na wakunga," amesema Mhe. Kingu
Wakati huo huo Mheshimiwa Kingu ameielekeza Wizara ya Afya kuendelea kuboresha mabaraza hayo kwa kuwa na mabaraza machache yenye ufanisi na tija pamoja na kuongeza rasilimali watu ili kupunguza uhaba wa wataalamu kwenye Sekta ya Afya.
"Tuwapongeze kwa wasilisho mliotoa, limetupa uelewa mpana kuhusu namna Mabaraza yanavyofanya kazi lakini pia tumeona kuna uhitaji mkubwa wa taalamu kutokana na wasilisho hilo ambalo lina onesha kuwa bado wahudumu hawatoshi.” Amesema Mhe. Kingu
Mhe. Kingu ametumia fursa hiyo kuyapongeza mabaraza yote mawili kwa namna yanavyo fuatilia kwa undani wataalam na kusimamia miiko na maadili pamoja na utaalamu na ubingwa bobevu.
“Sasa tumeelewa ni kwa namna gani wataalam wanapatikana, tuwapongeze tu kwa namna mnavyoendesha na ufatilia wataalam kabla ya kuwasajili na kuwapa leseni, hii itasaidia katika kutoa huduma tena zinazokidhi ubora kulingana na viwango vilivyopo.” Amesema Mhe. Kingu