Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MAAMBUKIZI YA UKIMWI KUTOKA MAMA KWENDA KWA MTOTO YAPUNGUA KUTOKA 1% HADI 0.3%

Posted on: November 23rd, 2024

Na WAF, Mwanza

Hali ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama mjamzito mwenye VVU kwenda kwa mtoto wakati wa kujifungua mkoani Mwanza yamepungua kutoka asilimia 1kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2024 na kufikia asilimia 0.3 kwa kipindi cha Julai hadi Septemba 2024.

Hayo yamebainishwa Novemba 21, 2024 jiji Mwanza na Mratibu wa UKIMWI mkoa wa Mwanza na magonjwa ya ngono na kifua kikuu (TB), Dkt. Kwadu Gloriosa Mashuda wakati wa ziara ya siku mbili ya timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais Tamisemi na Mfuko wa Dunia wa kupambana na Kifua Kikuu, UKIMWI na Malaria (Global Fund) kutoka Makao Makuu nchini Uswisi, iliyolenga kukagua miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Mfuko huo.

Dkt. Mashuda amesema mkoa wa Mwanza umefikia malengo ya kidunia ya “95 95 95” katika kutokomeza UKIMWI ambapo asilimia 95 ya wanaohisiwa kuwa na maambukizi wametambua hali yao ya maambukizi, huku asilimia tisa ya waligudulika na VVU wameanzishiwa dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI za ARV na asilimia 95 ya walio kwenye dawa za ARV wamefubaza virusi vya UKIMWI.

Kuhusu mwenendo wa ugonjwa wa kifua kikuu mkoani Mwanza, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Mashuda amefafanua kuwa, uibuaji wa watu wenye ugonjwa wa kifua kikuu umeonyesha mafanikio kuanzia kipindi cha Januari hadi Septemba 2024 ambapo mkoa umeweza kufikia lengo la zaidi ya asilimia 90

Naye Meneja wa Mpango wa Kudhibiti UKIMWI, Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini (NASHCoP) Dkt. Prosper Faustine amewashukuru wadau wa maendeleo katika sekta ya Afya na kusisitiza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo wakiwemo “Global Fund” ili kuimarisha huduma za afya nchini lengo likiwa ni kupunguza visa vipya vya maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI, Malaria na Kifua Kikuu kupitia utekelezaji wa afua mbali mbali.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwakilishi kutoka Mfuko wa Dunia “Global Fund” Dkt. Dan Koros ametoa rai kwa uongozi wa mkoa wa Mwanza kuongeza uhamasishaji wa kuzuia maambukizi mapya ya VVU kwa kuongeza upimaji binafsi VVU (HIV self-test) kwa wananchi.