Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MAAFISA USTAWI WA JAMII WASHAURI KUSHIRIKI KUTOA MAFUNZO

Posted on: November 16th, 2024

Maafisa Ustawi wa Jamii wameishauri Serikali kuona umuhimu wa kushiriki katika kutoa mafunzo kwa wahudumu ngazi ya jamii kwa kuwa wamekuwa wakifanya kazi na jamii.

Akizungumza Novemba 15, 2024 kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Njombe Afisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa huo Bi. Subilaga Mwaigwisya amesema hadi sasa wahudumu wa afya ngazi ya jamii 300 kati ya 900 wameanza mafunzo katika awamu ya kwanza, hivyo ni vyema maafisa Ustawi wa Jamii wakapata fursa ya kuwafundisha kwani wao wanaelewa vizuri mazingira ya jamii wanayoihudumia.

“Maafisa Ustawi wa Jamii tumekuwa tukifanya kazi kwa karibu na jamii, hivyo tukishirikishwa katika kutoa elimu kwa wahudumu wa afya ya jamii tutawapatia pia uzoefu wa kufanya kazi na jamii husika lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa wahudumu hao watakapohitimu wanatoa huduma bora kwa wananchi,” amefafanua Bi. Mwaigwisya.

Kiongozi wa timu ya Wataalamu na Mratibu wa Huduma za Afya ngazi ya Jamii kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Dkt May Alexander ambaye ameambatana na wataalamu kutoka Wizara ya Afya na mdau kutoka Taasisi ya Benjamin Mkapa, amesema kuwa Serikali kwa kuanzia imeanza kutoa mafunzo hayo kupitia vyuo vya afya vilivyopo katika mikoa husika na kwamba ujio wa wataalamu hao pamoja na kuangalia mchakato mzima wa kuwapata watoa huduma za afya katika jamii na jinsi mafunzo yanavyotolewa pia inapokea maoni na ushauri ambao utafanyiwa kazi kwa ajili ya maboresho ya mpango huo.

“Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa huduma za afya ngazi ya msingi zinaboreshwa ndiyo maana tunawapatia mafunzo wahudumu wa afya ngazi ya jamii ili wananchi wanufaike na huduma bora za afya zinazotolewa katika jamii inayowazunguka,” amefafanua Dkt. Alexander.

Wataalam hao wako mkoani Njombe kwa siku mbili ambapo watatembelea Halmashauri ya Mji wa Njombe na Makambako pamoja na vyuo vilivyopokea wanafunzi kwa ajili ya mafunzo maalumu ya wahudumu wa afya ngazi ya jamii katika halmashauri tajwa.