M-MAMA YAOKOA MAISHA, VIFO VYAPUNGUA
Posted on: January 16th, 2025
NA WAF-Dodoma
Serikali imefanikiwa kupunguza vifo vya watoto wachanga kwa kiwango kikubwa, huku mfumo wa usafiri wa dharura, M-Mama ukichangia kuokoa maisha ya akinamama na watoto wachanga nchini.
Akizungumza jijini Dodoma leo Januari 15, 2025 mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI kwenye ukumbi mdogo wa Bunge, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema kuwa vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano vimepungua kutoka 67 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2015/16 hadi 43 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2022.
“Tanzania ni miongoni mwa nchi chache zilizofanikiwa kufikia Malengo ya Milenia kwa kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano hadi angalau 54 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2015,” amesema Dkt. Mollel.
Dkt. Mollel ameeleza kuwa mfumo wa M-Mama, unaoratibu usafiri wa dharura kwa akinamama na watoto wachanga, umefanikiwa kuokoa maisha ya watu zaidi ya 5,000 tangu ulipoanzishwa. Zaidi ya akinamama na watoto wachanga 120,000 wamesafirishwa kwa dharura kupitia mfumo huo, hatua ambayo imeongeza mara mbili upatikanaji wa huduma za usafiri wa dharura katika maeneo yenye changamoto.
“Mfumo wa M-Mama umeondoa changamoto ya ukusanyaji wa data, ambapo awali taarifa za rufaa zilihifadhiwa ndani ya vitabu vya usajili kwenye vituo vya afya. Sasa taarifa hizi zinapatikana kwa urahisi kupitia mifumo yetu ya kidigitali,” ameongeza Dkt. Mollel.
Aidha, mfumo huo unatarajiwa kuwa na mafanikio makubwa zaidi, huku Wizara ya Afya ikipanga kuongeza uhamasishaji wa jamii na kuboresha zaidi huduma katika maeneo yenye mahitaji makubwa.
Pia, Dkt. Mollel amesema zaidi ya watoa huduma 20,000 wanapewa mafunzo rasmi na elekezi kazini kupitia mpango wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ili kuhakikisha huduma za afya kwa mama na mtoto zinaimarishwa.
Serikali imeahidi kuendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha huduma za afya kwa watoto wachanga na akina mama zinaboreshwa zaidi, huku lengo likiwa ni kupunguza vifo zaidi na kuimarisha ustawi wa familia nchini.