KONGAMANO LA KIMATAIFA LA TIBA UTALII KUFANYIKA 2026 DAR ES SALAAM
Posted on: September 19th, 2025
NA WAF - DAR ES SALAAM
Kongamano la Kimataifa la Tiba Utalii linatarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam mwaka 2026, lengo likiwa ni kuunganisha sekta ya afya na sekta ya utalii ili kuongeza thamani katika uchumi na kuboresha ubora wa huduma zinazotolewa nchini.
Hayo yameelezwa leo Septemba 18, 2025 na Mratibu wa Ushirikiano wa Umma na Sekta Binafsi wa Kanda, Dkt. Gunini Kamba wakati wa ufunguzi wa Kikao cha Maandalizi ya Kongamano la Tiba Utalii, Jijini Dar es salaam.
“Tanzania inajipanga kuwa kitovu cha tiba utalii barani Afrika. Hii ni fursa kwa taifa letu kuonesha uwezo tulionao katika huduma za kibingwa na ubora wa miundombinu ya afya,” amesema Dkt. Kamba.
“Tunatarajia wageni zaidi ya 1,000 kutoka mataifa mbalimbali duniani. Hii ni nafasi ya kipekee kwa sekta binafsi na umma kuonesha ubunifu na uwekezaji wao,” amesema Dkt. Kamba.
Dkt. Kamba amesema Serikali imewekeza zaidi katika hospitali za kitaifa na kanda, na sasa tunataka dunia ijionee matunda ya uwekezaji huo.
Kwa upande wake Mratibu wa Tiba Utalii Wizara ya Afya Dkt.Asha Mahita amesema Tiba utalii ni fursa ya kuongeza thamani ya utalii wetu. Tunapovutia watalii kwa huduma bora za afya, tunapanua wigo wa soko letu la utalii wa kimataifa.
“Tanzania siyo tu nchi ya vivutio vya asili, bali pia inakuwa kitovu cha tiba utalii. Kongamano hili litafungua milango ya uwekezaji na ushirikiano wa kimataifa,” amesema Dkt. Mahita.