KANDA YA MAGHARIBI KUPATA HOSPITALI YA KANDA
Posted on: July 9th, 2024
Na WAF, KIGOMA
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepanga kuanza ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Magharibi wilaya ya Ujiji mkoani Kigoma.
Kauli hiyo imebainishwa leo na Naibu Waziri wa Afya Dkt Godwin Mollel wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philipo Mpango, mkoani Kigoma wakati alipotembelea eneo litakalo jengwa mradi ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Magharibi na Chuo cha Afya na Sayansi shirikishi Muhimbili (MUHAS) - Kampasi ya Kigoma
Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2024/25 imetenga kiasi cha fedha Sh. bilioni nne kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi hospitali hiyo ya Rufaa ya kanda Magharibi.
"Usanifu wa michoro ya ujenzi wa Hospitali hiyo ulianza February 2024 na sasa upo katika hatua za mwisho za ukamilishaji ili ifikapo Julai 30, 2024 uwe umekamilika". amesema Dkt. Mollel
Akielezea eneo lilitengwa Mollel amesema Hekta 26.8 sawa na Ekari 66.2 ambazo zinapatikana Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Ameongeza kuwa ujenzi wa hospitali hiyo unatarajiwa kuanza mwanzoni mwa mwezi Novemba, 2024 baada ya kazi ya ubunifu wa michoro ya na zabuni ya kumpata mkandarasi wa ujenzi wa awamu ya kwanza kukamilika.
Vilevile ameongeza kuwa awamu ya kwanza ya mradi wa ujenzi wa hospitali
kazi ya ubunifu na usanifu wa michoro inatekelezwa na Mshauri Elekezi, Kampuni Y&P Architects (T) Ltd kutoka Dar es salaam akishirikiana na Kampuni tanzu za Donmark (T) Limited kama wakadiriaji majenzi, Agreneb Consult Limited kama Wahandisi washauri wa umeme na mitambo, na Lomo Consult Limited kama Wahandisi miundo (Service Engineers).
Usanifu na ubunifu wa awamu ya kwanza ya mradi huo wa ujenzi wa Hospitali ya Kanda ya Magharibi - Kigoma unahusisha jengo la wagonjwa wa nje na huduma ya dharura-OPD/EMD Complex
Jengo la huduma za uchunguzi na utambuzi wa magonjwa -Diagnostic Service Complex.
Pia, eneo jingine ni ujenzi wa jengo la huduma za Dawa – Pharmaceutical Services Block, jengo la Upasuaji - Surgical Complex, jengo la Mama na Mtoto- Maternity Complex.
Lakini pia majengo mengine ni jengo la Wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu- Intensive Care Unit Block,jengo la utawala- Administration Complex, jengo la kutakasia vifaa tiba- Central Sterile Supply Department (CSSD), jengo la kufulia- Laundry,jengo la kuhifadhia Maiti- Mortuary,jengo la kuchomea taka hatarishi- Incinerator,uzio, njia za kupita wagonjwa na mazingira ya nje.
Amesisitiza kuwa mradi huo mkubwa na wa kimkakati ni miongoni mwa vielelezo vingi vya juhudi kubwa zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa na serikali ya awamu ya sita katika kuboresha sekta ya afya katika maeneo yote ya nchi.
“Wizara ya Afya inapenda kutoa pongezi na shukrani za dhati kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujumla kwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimaendeleo yenye lengo la kuboresha huduma za afya nchini”ameshukuru Dkt Mollel
Hata hivyo, amesema kipekee anaushukuru uongozi wa mkoa wa Kigoma, hususan mkuu wa mkoa Thobias Andengenye na Katibu Tawala wa Mkoa, Hassan Abbas Rugwa kwa ufuatiliaji wa karibu wa kila hatua ya utekelezaji wa mradi hup mkubwa na miradi mingine mingi inayoendelea kutekelezwa.
Kuhusu mipaka ya eneo husika Mollel amesema kimepakana na Chuo cha Afya na Sayansi shirikishi Muhimbili (MUHAS) - Kampasi ya Kigoma kwa upande wa kaskazini, ili hali upande wa Mashariki likipakana na Kiwanda cha asali cha Upendo, wakati Reli ya Kigoma kutokea Dar es salaam ikipakana na eneo hilo kwa upande wa Magharibi na makazi ya watu yakipakana na eneo hilo kwa upande wa Kusini.
MWISHO