KAMILISHENI MIKAKATI YA LISHE ILI KUONDOA UDUMAVU NCHINI- BUNGE
Posted on: August 14th, 2024
Na WAF - DODOMA
Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya bunge ya afya na masuala ya UKIMWI Mhe. Elibariki Kingu (MB) ameitaka Wizara ya Afya kuendelea kutekeleza mikakati na mipango iliyojiwekea kwa haraka ya kuimarisha lishe nchini ili kuondoa tatizo la udumavu na utapia mlo uliokithiri.
Mhe. Kingu ameyasema hayo leo Agosti 13, 2024 wakati wa kikao cha kamati ya kudumu ya Bunge ya Afya na masuala ya UKIMWI baada ya wasilisho la mpango kazi wa Wizara ya Afya, juu mikakati na mipango ya kuimarisha lishe nchini.
“Tumepokea wasilisho lenu ni zuri, kwani limeondoa wasiwasi kwa wajumbe kuhusu ajenda ya lishe, lakini mikakati iliyopangwa ikatekelezwe kwa uharaka ili kupata matokeo na kuondoa matatizo yatokanayo na lishe duni” amesema Mhe. Kingu
Aidha, Mhe. Kingu ameielekeza wizara ya afya kuongeza wigo wa utoaji elimu ya lishe kwa wananchi ikiwemo kutumia vyombo vya habari ili kupunguza tatizo la udumavu nchini.
Kwa upande wake Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema, mkakati huu umegawanyika katika vipaumbele vikuu vinne ili kuleta ufanisi na matokeo ya haraka kwa lengo la kupunguza udumavu nchini.
“Utekelezaji wa majukumu una maeneo manne ambayo ni uhamasishaji jamii kuhusu unyonyeshaji maziwa ya mama kwa mtoto, utoaji wa matone ya Vitamini 'A' kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, kuimarisha upatikanaji wa virutubishi na kutoa elimu ya lishe na uhamasishaji wa masuala ya ulaji unaofaa”. Amesema waziri Ummy.
Hata hivyo, Waziri Ummy ameishukuru kamati ya kudumu ya bunge ya afya na maswala ya UKIMWI kwa kupokea vipaumbele hivyo na kuvijadili kwa lengo la kuifanya jamii iwe na afya bora na kuondokana na magonjwa nyemelezi ya kuambukizwa na yasio ya kuambukiza.
“Elimu ya lishe inatakiwa itolewe katika nyaja zote, kwani watanzania hawali mbogamboga, na virutubisho vingine, pia hata mashuleni kuwe na vioski vinavyouza vyakula vyenye virutubisho na sio kuuza vitu visivyo na manufaa kwenye afya ya watoto”. Amesema Waziri Ummy.