Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

KAMBI YA UPASUAJI MTOTO WA JICHO IRINGA, KUWAFIKIA WATU ZAIDI YA 700

Posted on: August 4th, 2025

Na WAF, Iringa


Watu wapatao 120 katika siku ya kwanza wamefikiwa na huduma ya upasuaji wa mtoto wa jicho katika kambi ya matibabu ya ugonjwa huo inayoendeshwa na waataalam wa afya ya macho wakiwemo madaktari  bingwa wabobobezi kutoka hospitali za nyanda za juu kusini, katika kituo cha Afya Isimani mkoani Iringa.


Kambi hiyo inayoendelea kwa siku saba (7) katika kituo hicho  inatarajia kufanya upasuaji kwa watu  kati ya 600 hadi 700 kwa siku sita baada ya watu wengi kujitokeza kutoka maeneo ya Iringa vijijini na maeneo jirani kuchangankia huduma hiyo inayotolewa na Serikali kwa ushirikiano na Shirika la Kimataifa la Hellen Keller.


Akiongea mara baada ya kufanyiwa usuaji wa ugonjwa wa mtoto wa jicho Bi. Nuru Mathias Kayage, amesema amekuwa akiishi na ugonjwa huo tangu mwaka 2021 hali ambayo imechangia kuvunjika kwa ndoa yake kutokana na kuwa na uoni hafifu lakini sasa amekuwa na matumaini mapya baada ya kuanza kuona upya kufuatia tiba ya upasuaji wa mtoto wa jicho.


‘’Nimepitia kipindi kigumu mpaka ndugu jamaa na marafiki walikuwa wananitenga hata nilipokuwa nawatembelea ndugu walikuwa wanadhani naenda kuomba msaada, kutokana na changamoto hii nilitelekezwa na mume nikiwa na watoto watatu, sijui niwashukru vipi walioleta msaada huu, sina chakuwalipa, Mungu awabariki sana,’’ amesema Bi. Matiasi.


Awali Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Khery James  akiukaribisha ujumbe wa Bodi ya Wataalam kutoka Hellen Keller Ofisini kwake  amelishukuru shirika hilo kwa kutoa msaada wa vifaa kila vinapoitajika, kutoa utaalam kwa madaktari wenyeji na kuendeleza ushirikiano kati yao na Serikali.


Mkuu huyo wa Mkoa amesema lengo la ujumbe wa Hellen Keller mkoani Iringa ni kujionea namna gani huduma wanazofadhili zinavyofanya kazi ikiwemo kujadiliana kwa pamoja maeneo mengine ya ushirikiano kwani shirika hilo limekuwepo hapa nchini kwa zaidi ya miaka 30.


Naye rais wa Shiriko hilo Duniani Sarah Bochie ameuambia ujumbe wa Mkuu wa Mkoa wa Iringa kuwa shirika lake liko mkoani Iringa ili kujionea huduma zinazotolewa kwa vitendo kwani shirika lake linafanya kazi kwa kanzi data na takwimu ili kutoa tathimini ya huduma zake.



Ujumbe huo kabla ya kwenda mkoani Iringa Agosti 4, 2025  ulikutana na Menejimenti ya Wizara jijini Dodoma.