Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

KAMBI YA MADAKTARI BINGWA KUIMARISHA HUDUMA BORA ZA AFYA NGAZI YA MSINGI ARUSHA

Posted on: May 20th, 2024Kambi ya Madaktari bingwa wa Rais Samia inaenda kuimarisha huduma bora za afya kwa wananchi kupitia maboresho makubwa katika miundombinu na vifaa tiba hivyo kurahisisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi ngazi ya Halmashauri mkoani Arusha.


Akizindua Kambi hiyo Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha Ndg. Apolinary Andrew, leo Mei 20, 2024 ameeleza Kambi hiyo inaendana na maboresho yaliofanyika kwenye Sekta ya Afya ndani ya Mkoa wa Arusha hususani kwenye upatikanaji wa miundo mbinu, vifaa tiba pamoja na dawa hali itakayopelekea kurahisisha ufanisi wa kazi kwa Madaktari Bingwa/Bingwa bobezi


Aidha Ndg Andrew amesema kuwa kambi hiyo ya Madaktari Bingwa wa Mama Samia inalenga kusogeza huduma bora za Afya kwa Wananchi wa Mkoa wa Arusha kwa kuleta huduma za Matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi kwa gharama nafuu kwa Wananchi waliopo mbali na upatikanaji wa huduma hizo na kuboresha upatikanaji wa huduma za Afya maeneo hayo.


Hata hivyo amesema madaktari bingwa 35 wa fani mbalimbali za Afya wataweka kambi za matibabu katika Halmashauri za Wilaya zote za Mkoa wa Arusha kwa muda wa siku tano kuanzia Mei 20, 2024 hadi Mei 24, 2024 na kutoa huduma za Kitabibu kwa Wananchi wa maeneo husika pamoja na kutoa mafunzo kwa Watumishi wa Hospitali za Wilaya.


Akiongea, Afisa Programu Wizara ya Afya, Dkt. Joachim Masunga ameeleza kuwa wamefika Mkoa wa Arusha wakiongozana na Madaktari Bingwa kutoka hospitali mbalimbali Nchini kwa lengo la kutoa huduma za Kitabibu za Kibingwa na Bingwa bobezi kwa Wananchi na kuwezesha kuwafikishia huduma hizi karibu na maeneo yao wanayoishi na kuwapunguzia gharama za kuzifuata mbali.


Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Afya imeandaa Kampeni hiyo ambayo itafikia Halmashuri zote 184 na hospitali zote za Wilaya Nchi Nzima kwa kupeleka huduma za Kitabibu za Kibingwa kwa kutumia Madaktari Bingwa wa Mama Samia ikiwa ni awamu ya Nne toka zoezi limeanza.