Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

KAMBI MAALUM YA HUDUMA ZA MATIBABU YA KIBINGWA KUIFIKIA KANDA SITA NCHINI.

Posted on: April 29th, 2024



Na WAF - Dodoma

Wizara ya Afya imeanza utekelezaji wa huduma za kibingwa za Mkoba katika kambi sita kwenye mikoa sita Nchini hii ikiwa ni azma ya Serikali ya awamu ya sita kufikisha huduma za afya karibu na wananchi.

Kwa mujibu taarifa iliyotolewa kwa umma Aprili 29, 2024, na Wizara ya Afya na kusainiwa na Kaimu Mkuu Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali Bw. Englibert Kayombo imesema mikoa hiyo ni Geita, Morogoro, Lindi, Songea, Tanga na Kigoma. Ambapo Madaktari bingwa kutoka katika hospitali za rufaa za Mikoa, Kanda, Taifa na Maalum watashiriki kutoa huduma 12 za kibingwa na Ubingwa Bobezi.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa Malengo makuu ya huduma hizo za Mkoba ni pamoja na Kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi.

"Shabaha ni kuwajengea uwezo wataalamu wa fani mbali mbali waliopo ngazi zote za kutolea huduma na kuibua wagonjwa wanaohitaji huduma za ubingwa bobezi katika hospitali za Kanda, Maalum na Taifa" imeeleza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo huduma za kibingwa zitakazotolewa na Madaktari hao ni pamoja na Ubingwa wa akina mama na uzazi, watoto, Upasuaji, Magonjwa ya ndani, Upasuaji Mifupa, Dharura na ajali, Radiolojia, Utoaji wa dawa za ganzi na usingizi, Afya ya akili, huduma za Utengemao, huduma za Macho na huduma za kinywa na Meno.

"Kambi hizi zinafanyika kuanzia tarehe 29 April mpaka tarehe 11 Mei, 2024 kuanzia saa 2 asubuhi mpaka saa 10 jioni. Kampeni hii itafanyika kwa awamu mbili, na kila awamu itadumu kwa muda wa juma moja.

Awamu ya kwanza itafanyika katika Mikoa ya Geita, Ruvuma na Tanga kuanzia tarehe 29 Aprili hadi tarehe 4 Mei, 2024 na awamu ya pili itafanyika katika Mikoa ya Lindi, Morogoro na Kigoma kuanzia tarehe 06-11 Mei, 2024" amesema Kayombo.

Sambamba na kambi hizo za Madaktari Bingwa wa Rais, Dkt Samia katika Hospitali za Mikoa, Wizara pia inaendelea kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI kuendeleza Kampeni ya kuimarisha ubora wa huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto kwenye ngazi za Halmashauri na baadhi ya vituo vya afya nchini kupitia kampeni ya Madaktari bingwa wa Mama.