Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

KAMATI YARIDHISHWA NA HATUA ZA UTEKELEZAJI WA BIMA YA AFYA KWA WOTE

Posted on: January 19th, 2026

Na, WAF-Dodoma

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Afya na Masuala ya UKIMWI, Dkt. Johannes Lukumay amesema kamati imeridhishwa na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, akibainisha kuwa mwelekeo huo unaonesha utayari wa Taifa kuelekea uzinduzi kamili wa mfumo huo.

Dkt. Lukumay ametoa kauli hiyo leo Januari 19, 2026, bungeni jijini Dodoma, wakati wa kikao cha kamati hiyo kilicholenga kusikiliza wasilisho la hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote.

Amesema maendeleo yaliyopo yanaonesha dhamira ya Serikali kuhakikisha kila Mtanzania anapata haki ya huduma za afya kupitia mfumo jumuishi wa bima.

Hata hivyo, Dkt. Lukumay ameitaka Wizara ya Afya kuongeza kasi ya ufuatiliaji na utekelezaji wa mpango huo ili kurahisisha na kuharakisha upatikanaji wa huduma za bima ya afya kwa wananchi, sambamba na kuondoa changamoto zinazoweza kujitokeza katika utekelezaji wake.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuchukua hatua madhubuti kuboresha na kuhakikisha Bima ya Afya kwa Wote inaanza kutekelezwa kikamilifu, kama ilivyoainishwa katika ahadi ya Rais wakati wa kampeni.

Dkt. Samizi amewaomba wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge kuendelea kutoa ushirikiano kwa Wizara pamoja na kushiriki kikamilifu katika kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa Bima ya Afya kwa Wote. Amesema utekelezaji wa mpango huo umeanza na utazinduliwa rasmi Februari mwaka huu, hatua inayolenga kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wote.

Ameongeza kuwa ushirikiano wa pamoja kati ya Serikali, bunge na wananchi ni muhimu katika kuhakikisha mafanikio na uendelevu wa Bima ya Afya kwa Wote nchini.