KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA KASI YA UJENZI WA VIWANDA VYA DAWA NCHINI
Posted on: October 24th, 2026Na Shaban Juma, WAF – Dar es Salaam
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Dkt. Zeyana Hamid, imeridhishwa na kasi ya ujenzi wa viwanda vya dawa nchini, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji wa dawa ndani ya nchi na kupunguza utegemezi wa dawa kutoka nje.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo jijini Dar es Salaam, leo Oktoba 24, 2026, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imedhamiria kuimarisha uzalishaji wa dawa nchini kupitia ujenzi na uendelezaji wa viwanda vya dawa.
Amesema kasi inayoendelea katika ujenzi wa viwanda hivyo inaonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha nchi inaimarisha uwezo wake wa kuzalisha dawa zinazohitajika katika vituo vya kutolea huduma za afya, pamoja na kupunguza gharama za uagizaji wa dawa kutoka nje ya nchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dkt. Zeyana Hamid, amesisitiza umuhimu wa viwanda vinavyojengwa nchini kutoa kipaumbele kwa ajira za Watanzania ili wananchi wanufaike kiuchumi na kuchangia ongezeko la kipato cha kaya pamoja na kukuza uchumi wa taifa.
Aidha, ameshauri katika ujenzi wa viwanda hivyo kuzingatiwa matumizi ya malighafi na vifaa vya ujenzi vinavyopatikana nchini, badala ya kuagiza kutoka nje, hatua itakayosaidia kukuza soko la bidhaa za ndani, kuongeza mzunguko wa fedha nchini na kupunguza gharama za ujenzi.
Vilevile, Kamati imeishauri Serikali kuangalia namna bora ya kuhakikisha kunakuwa na soko la uhakika la dawa zinazozalishwa nchini, ili viwanda hivyo viweze kuuza bidhaa zake, kujiendesha kwa ufanisi na kuendelea kuongeza uzalishaji. Hatua hiyo pia inalenga kuhakikisha uwekezaji unaofanyika unakuwa na tija na unachangia upatikanaji endelevu wa dawa kwa wananchi.
Kamati imeeleza kuwa kuimarisha viwanda vya dawa nchini ni hatua muhimu katika kujenga uwezo wa ndani wa uzalishaji, kukuza ajira na kuhakikisha sekta ya afya inakuwa na upatikanaji wa dawa wa uhakika kwa ajili ya kutoa huduma bora kwa Watanzania.