Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

KAMATI YA BUNGE YA HUDUMA NA MAENDELEO YA JAMII YAIPONGEZA SERIKALI KWA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA AFYA KATIKA HOSPITALI YA RUFAA MKOA WA MBEYA

Posted on: March 18th, 2022Na WAF - Mbeya.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, imeipongeza Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kutenga fedha
nyingi kwa ajili ya miradi ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya kutolea huduma za Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Stanslaus Nyongo mara baada ya Kamati hiyo kufanya ziara katika Hospitali
ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya na kukagua miradi ya ujenzi wa Jengo la Upasuaji, ukarabati wa wodi ya wagoniwa mahututi pamoja na jengo la huduma za dharura.

"Tumeona hapa katika Mkoa wa Mbeya fedha nyingi zimekuja kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la Upasuaji zaidi ya Bilioni 5, na fedha nyingine zimekuja kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la kutolea huduma za dharura pamoja na ukarabati wa wodi ya wagonjwa mahututi" amesema Mhe. Nyongo.

Hata hivyo Kamati hiyo pia imeishauri Serikali kuboresha huduma zaidi za afya na kuondoa changamoto zilizopo ikiwemo uhaba wa dawa pamoja na wataalam wa kutosha katika vituo vya kutolea huduma.

Awali akitoa taarifa ya Hospitali mbele ya Kamati hiyo Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya Dkt. Alinanuswe Kasililika amesema kuwa wamepokea kiasi cha Shilingi Bilioni 5.3 kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la Upasuaji ambapo ujenzi umefikia asilimia 88 na unatarajiwa kukamilika tarehe 4 mwezi Aprili 2022.

Ameendelea kwa kusema pia walipokea Shilingi Milioni 150 kwa ajili ya ukarabati wa wodi ya wagonjwa mahututi, huku ujenzi wa jengo la huduma za dharula ukifikia asilimia 99.9 ambao umegharimu kiasi cha Shilingi Milioni 877 zilizotolewa na Global Fund.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha huduma za afya kwa kuhakikisha kunakuwa na miundombinu ya kutosha ya kutolea huduma za afya, kuboresha upatikanaji wa dawa pamoja na wataalam.

Dkt. Mollel ameutaka Uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya kuwa na ratiba ya kuripoti taarifa zao kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya kwa ajili ya kuboresha zaidi usimamizi wa shughuli za Sekta ya Afya ndani ya Mkoa.

Nyinyi hapa ni watumishi wa Wizara ya Afya lakini mpo huku ngazi ya Mkoa na Wilaya, tunawataka muwe nmaripoti moja kwa moja kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa ajili ya kuboresha usimamizi wa miradi mbalimbali" amesema Dkt. Mollel.