JKCI YATEKELEZA DIRA YA TAIFA 2050 KUPITIA UWEKEZAJI WA HUDUMA BINGWA ZA AFYA
Posted on: July 10th, 2026Na Hassan Kimweri, WAF - Dar es Salaam
Uwekezaji unaoendelea katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ni utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 inayolenga kuimarisha huduma katika sekta ya afya, kukuza uchumi na kuboresha ustawi wa wananchi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Mkumbo amesema hayo leo Julai 10, 2026, wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la Jengo la Tiba ya Michezo kwa ajili ya maandalizi ya AFCON 2027 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dar Group, jijini Dar es Salaam.
"Dira ya Taifa ya mwaka 2050 imeweka kipaumbele katika kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana kwa wote pamoja na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha tiba utalii, wananchi na wageni kutoka nje ya nchi watapata huduma za kibingwa ndani ya Tanzania," amesema Prof. Mkumbo
Aidha, Prof. Mkumbo amesema maboresho yaliyofanywa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yamechangia kupunguza idadi ya Watanzania waliokuwa wakisafiri nje ya nchi kwa matibabu, hatua iliyookoa fedha nyingi za kigeni ambazo sasa zinabaki nchini na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Amesema, Serikali imewekeza takribani shilingi bilioni 18 katika ujenzi wa jengo hilo la tiba ya michezo, uwekezaji ambao utasaidia kuimarisha maandalizi ya AFCON 2027 pamoja na kupanua huduma za kibingwa kwa wanamichezo na wananchi kwa ujumla.
Pia, Prof. Mkumbo amesema Serikali inaendelea kuimarisha taasisi na mashirika ya umma kwa kuvipa uhuru wa kufanya kazi kwa kuzingatia malengo na viashiria vya utendaji ili viweze kutoa huduma bora huku vikichangia maendeleo ya uchumi wa taifa.
Akimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge, Prof. Mkumbo amesema taasisi hiyo imeonyesha mafanikio makubwa kutokana na uongozi wenye maono, ushirikiano mzuri wa watumishi pamoja na uwekezaji unaoendelea katika huduma za kibingwa za afya.