JENGO LA TIBA LA WATOTO WACHANGA KUPUNGUZA RUFAA KWA ZAIDI YA KM 100
Posted on: October 16th, 2023Na WAF, Dar Es Salaam.
Mashirika na Taasisi zisizo za kiserikali za JHPIEGO na Doris Foundation zimeazimia kujenga jengo la tiba la Watoto wachanga katika hospitali ya Kwimba ili kupunguza Rufaa ya Watoto wachanga KM 100 na kuwepesishia Huduma za matibabu.
Haya yameelezwa na mkurugenzi wa Huduma za mama na mtoto Dkt. Ahmad Makuwani aliposhiriki mbio za hisani zinazofahamika kwa jina la ‘Miles for Mothers’ mkoani Dar es Salaam zinazolenga kuchangia kwa ajili ya ujezi wa jengo la tiba kwa Watoto wachanga kwenye hospitali ya Kwimba iliyopo mkoani Mwanza.
“Kwa mujibu wa takwimu, takribani Watoto 18,073 huzaliwa kila mwaka katika hospitali hii ya Kwimba. Na katika hao, asilimia 7 huwa ni Watoto waliozaliwa na uzito pungufu maarufu kama Watoto njiti. Watoto wachanga wakiuguwa ama kuzidiwa, hupatiwa rufaa kwenda takribani kilomita 100 ambapo ndipo kuna hospitali ya karibu ya rufaa. Ukiangalia umbali na gharama, kwa familia nyingi inakuwa ni mzigo mzito wa kiuchumi na hivyo wengi hukwama kwenye kutekeleza hili”. Ameeleza Dkt. Makuwani.
Aidha Dkt. Makuwani amesema kuwa kupitia ushirikiano kutoka katika mashirika hayo kama JHPIEGO na Doris Foundation Serikali inafarijika kwa hatua ambazo zinaiwezesha kufikia malengo ya maboresho ya Huduma bora za afya kwa wananchi.
“Nitumie fursa hii kutoa rai kwa mashirika mengine na taasisi zisizo za kiserikali kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita za kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za Afya kwa kila mtanzania”. Amesema Dkt. Makuwani.
Sambamba na hilo Dkt. Makuwani ameyashuruku mashirika hayo kwa kujitoa kwao kuweza kuisaidia Serikali na wananchi kwa ujumla katika upatikanaji wa Huduma bora za afya nchini kwa kuwawezesha Wananchi kutosafiri umbali mrefu kufata Huduma za afya.
“Serikali inaendelea kufanya maboresho makubwa kwenye sekta ya Afya na pale ambapo wadau kama Jhpiego na Doris Mollel Foundation wanapoona tija kuunga mkono juhudi hizi ni wazi kwamba sisi kama taifa tunafarijika mno na tunafahamu kwa ushirkiano huu tunapiga hatua kubwa kiurahisi kwenye kufikia malengo ya nchi yetu”. Ameelezea Dkt. Makuwani.