Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

“JAMII IKIELIMIKA TUTATOKOMEZA MALARIA IFIKAPO 2030”- DKT. KIKWETE

Posted on: March 26th, 2024



Na WAF-DSM

Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete amesema unyunyuziaji wa dawa kuuwa mazalia ya mbu, kutoa elimu kwa wananchi juu matumizi sahihi ya vyandarua pamoja na kupulizia dawa ndani ya nyumba itaiwezesha nchi kufikia malengo ya kutokemeza ugonjwa wa Malaria ifikapo 2030 kama mkataba wa nchi wanachama zinazokabiliana na malaria unavyoelekeza.

Dkt. Kikwete, amesema hayo Machi 26,2024 jijini Dar es Salaam kwenye kikao cha pamoja na wajumbe hao wakati wa mkutano wa tatu wa kamati ya kitaifa iliyoundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kukabiliana na Malaria.

Dkt. Kikwete amesema Tanzania inatajwa kuwa nchi ya 11 kwenye nchi zenye maambukizi ya malaria na vifo vitokanavyo na malaria kote duniani imejiwekea malengo ya kutokomeza ugonjwa huo ifikapo 2030, na yeye akiwa mmoja ya wajumbe wanaounda mtandao wa Dunia wa kutokomeza Malaria anaona fahari kwa hatua zinazochukuliwa na nchi ya Tanzania.

Kikwete amefafanua kuwa mwaka 2023 miongoni mwa watanzania milioni 19.8 waliofanyiwa vipimo vya malaria miongoni mwao milioni 3.46 walibainika kuwa na malaria ikilinganishwa na mwaka 2022 ambapo waliopimwa walikuwa 18.6 na waliobainika kuwa na malaria walikuwa milioni 3.56 ili hali katika vipimo vya 2021 jumla ya watanzania milioni 20.2 waliopimwa na watu milioni 4.4 walikuwa wameambukizwa malaria.

“Vifo vilivyotokana na malaria kwa mwaka 2023 vilikuwa 1,540 ikilinganishwa na vifo 1,735 vya mwaka 2022 hali ambayo ni tofauti na mwaka 2021 ambapo vifo vilikuwa 1,882”. Amesema Dkt. Kikwete.

Akiongea kwenye Mkutano huo, Mwenyekiti wa Kamati ya kitaifa ya kukabiliana na Malaria, Leodgar Tenga amesema njia pekee yakufanikiwa kukabiliana na kufikia malengo ya kutokomeza ugonjwa huo ni kushirikisha makundi yenye ushawishi ndani ya jamii wakiwepo viongozi wa dini na wanamichezo kwa kuwapatia maudhui na wao kuyasambaza kwa jamii ya kitanzania.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Miradi kutoka Wizara ya Afya Dkt. Catherine Joachim amesema wataendelea kushirikiana ipasavyo na wadau wote ili dhana ya Tanzania bila malaria ifikapo 2030 iweze kufanikiwa.