HUDUMA ZA UTENGEMAO NI MUHIMU KATIKA KUBORESHA, KUIMARISHA HUDUMA ZA AFYA NCHINI.
Posted on: September 6th, 2025
Na WAF - Dar es Salaam,
Serikali kupitia Wizara ya Afya imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kuimarisha huduma za utengamao kama sehemu muhimu ya mfumo wa afya nchini.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Septemba 4, 2025 Jijini Dar es Salaam kuelekea Kongamano la Tatu la Utengamao 2025, Dkt. Hamad Nyembea amesema huduma za utengamao zina mchango mkubwa katika kusaidia wagonjwa waliopata majeraha, magonjwa ya muda mrefu na changamoto za kisaikolojia ili warejee katika hali ya kawaida na kuboresha maisha yao.
“Kongamano hili lina kaulimbiu isemayo ‘Ubia na Ushirikiano ni Muhimu katika Kuimarisha Utoaji wa Huduma za Utengamao’ na linalenga kuwakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo wataalam wa afya, watunga sera, wawakilishi wa mashirika yasiyo ya kiserikali na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa ajili ya kujadili mbinu bora za kuimarisha huduma hizi,” amesema Dkt. Nyembea.
Aidha, amebainisha kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya atahudhuria kongamano hilo kama Mgeni Rasmi, hatua inayoonesha msisitizo wa serikali katika kuboresha huduma za afya.
Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha huduma za utengamao zinawafikia wananchi wengi zaidi, hususan vijijini na maeneo yenye uhaba wa huduma.
“Tunatambua kwamba hakuna maendeleo ya kweli bila afya bora, na afya bora haiwezi kufikiwa bila huduma za utengamao zinazowawezesha wananchi kurejea katika hali ya kawaida baada ya maradhi au majeraha,” amesisitiza Dkt. Nyembea.
Kongamano hilo la mwaka litatoa fursa ya kubadilishana uzoefu, maarifa na mikakati ya kuimarisha huduma za utengamao nchini Tanzania, huku Wizara ikiahidi kuendelea kuwa bega kwa bega na wadau wote katika safari ya kujenga taifa lenye afya bora kwa wote.
Kongamano la tatu la Utengemao linaloandaliwa na Rehab Health
Kwa ushirikiano na Wizara ya Afya na Jumuiya ya East, Central and Southern Africa Health Community (ECSA-HC) linatarajiwa kufanyika kuanzia Septemba 10 hadi 12, 2025 Katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere Convention Centre (JNICC).