Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

HUDUMA ZA UTENGAMAO ZINA MCHANGO CHANYA KATIKA KUIMARISHA MFUMO WA AFYA

Posted on: September 11th, 2024

Na WAF - DAR ES SALAAM


Huduma za utengamao zimetajwa kuwa na mchango katika kuimarisha mfumo wa afya kwa kusaidia wagonjwa walio na majeraha pamoja na wenye magonjwa ya muda mrefu kurejea katika hali ya kawaida kwa kuwatibu na kuboresha wa maisha yao.


Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Wizara ya Afya Dkt. Hamad Nyembea Septemba 11, 2024 Jijini Dar es salam wakati wa Mkutano na wanahabari kuhusu kongamano la utengamao linalotarajiwa kufanyika Septemba 18-20, 2024 Jijini Dar es salaam linaloandaliwa na Taasisi ya Rehab Health.


Dkt. Nyembea amesema katika kuhakikisha huduma za afya zinakuwa bora na zenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya Watanzania wote, utengamao ni sehemu muhimu kwani unatoa msaada kwa wagonjwa wanaohitaji huduma za urekebishaji wa viungo. 


“Wizara ya Afya inatambua na kuthamini sana mchango wa huduma za utengamao katika kuimarisha mfumo wa afya wa nchi yetu na huduma hizi ni sehemu muhimu ya kutibu na kusaidia wagonjwa walio

na majeraha au magonjwa ya muda mrefu na kuwasaidia kurejea katika hali ya kawaida na kuboresha ubora wa maisha yao”. Amesema Dkt. Nyembea.


Amesema Serikali imekuwa ikiweka msisitizo mkubwa katika kuhakikisha huduma za afya za utengamao zinakuwa bora na zenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya Watanzania wote bila kujali hali zao au maeneo wanakoishi kwani imekua ni sehemu muhimu kwa wagonjwa wanaohitaji huduma za urekebishaji wa viungo, matibabu ya muda mrefu na msaada wa kisaikolojia ili waweze kurejea katika hali yao ya kawaida.


Ameongeza kuwa wadau mbalimbali wa sekta ya afya, watunga sera, wataalamu, na mashirika yasiyo ya kiserikali watapata fursa ya kujadili na kubadilishana mawazo

juu ya njia bora za kuimarisha huduma za utengamao nchini Tanzania kwa pamoja na Waziri mwenye dhamana ya Afya nchini.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Rehab Health Remla Shirima amesema lengo la Kongamano hilo ni kuwakutanisha wataalam, watoa huduma za afya, watunga sera, na washirika mbalimbali ili kujadili mikakati ya kuendeleza huduma za utengamao nchini Tanzania. 


“Tunalenga kuimarisha mfumo wa afya kwa kuhakikisha huduma za utengamao zinafika katika ngazi za msingi za huduma za afya na jamii Pia, tunataka kubadilishana maarifa kuhusu utafiti wa hivi karibuni, uvumbuzi, na mbinu bora za kuboresha huduma za utengamao kwa wagonjwa”. Amesema Remla