Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

HUDUMA ZA UTENGAMAO KWA WATOTO WENYE USONJI KUBORESHWA - WAZIRI UMMY

Posted on: April 4th, 2024



Na. WAF - Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Afya imeanza kuchukua hatua madhubuti ili kuongeza nguvu katika uboreshaji na upatikanaji wa huduma za Utengamao kwa watoto wenye Usonji pamoja na watoto wenye ulemavu ikiwemo kuongeza idadi ya wataalamu wa huduma za Saikolojia Tiba (Clinical Psychology).

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema hayo leo Aprili 3, 2024 kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii (X, Instagram) baada ya kumsikiliza Mzazi wa mtoto mwenye Usonji Bi. Hamida Michael aliyerekodiwa na Azam Tv.

“Nimeguswa na taarifa hii ya Mama Hudhaifa na hali hi inawakabili wazazi wengi nchini kwetu hususani wanawake wanaolea watoto wenye Ulemavu ikiwemo Watoto wenye Usonji.” Amesema Waziri Ummy

Amesema, ni kweli bado Tanzania haijafanya vizuri sana katika upatikanaji wa huduma za utengamao hususani kwa watoto ikiwemo watoto wenye Usonji pamoja na watoto wenye ulemavu kwa ujumla, lakini Serikali inaendelea na juhudi mbalimbali ili kuboresha huduma hizo.

“Tumeanza kuchukua hatua mahususi ili kuongeza nguvu za kuboresha na kusogeza upatikanaji wa huduma za Utengamao kwa watoto wenye usonji na watoto wenye ulemavu kwa ujumla ikiwemo kuongeza idadi ya wataalamu wa huduma za Utengamao hususani Huduma za Saikolojia Tiba (Clinical Psychology).” Amesema Waziri Ummy

Amesema, hatua nyingine zinazochukuliwa ni pamoja na mazoezi tiba (Physiotherapy), mazoezi kazi (Occupational Therapy), huduma za mawasiliano na kuongea (Speech and Communication Therapy) sambamba na kuweka miundombinu na Vifaa Tiba kwa ajili ya huduma za Utengamao kwa watoto, wazee na watoto waliopata Kiharusi.

Waziri Ummy ametoa pongezi kwa Chuo Kikuu cha Afya Muhimbili kwa kuanzisha kozi mbalimbali za ngazi ya Shahada ya kwanza (Degree) katika Huduma za Utengamao na Afya ya Akili ambayo itasaidia kupunguza tatizo la Usonji nchini.

“Naamini hatua tulizoanza kuzichukua zitatuwezesha kuwafikia watoto wengi ili waishi maisha bora zaidi na kuweza kujitegemea na kushiriki katika shughuli za uzalishaji Mali.” Amesema Waziri Ummy