HUDUMA ZA AFYA YA KINYWA NA MENO ZAFIKIA ASILIMIA 43 KATIKA VITUO NCHINI
Posted on: October 26th, 2026Na Atley Kuni, WAF-DODOMA
Serikali imesema wigo wa vituo vinavyotoa huduma za afya ya kinywa na meno nchini umeongezeka kutoka asilimia 7 mwaka 2022 hadi asilimia 43 mwaka 2026, kiwango kilichovuka lengo la asilimia 20 lililokuwa limepangwa kufikiwa ifikapo mwaka 2030.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Afya na Lishe, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Dkt. Rashid Mfaume leo Oktoba 26, 2026 wakati akifungua Kikao Kazi cha Mwaka cha Madaktari wa Afya ya Kinywa na Meno wa Mikoa, kinachofanyika jijini Dodoma.
Dkt. Mfaume amesema kiwango cha uzibaji wa meno kimeongezeka kutoka asilimia 30 mwaka 2022 hadi asilimia 46.6 mwaka 2025, kikiongezeka kwa asilimia 16.6.
"Lengo ni kuhakikisha angalau asilimia 60 ya wananchi wenye meno yaliyooza wanapata huduma ya uzibaji badala ya kung’olewa, pale tathmini ya kitabibu inaporuhusu, huku akiagiza vituo vya kutolea huduma kufuatilia uwiano wa meno yanayotibiwa na yanayong’olewa.
Katika hatua nyingine, amesema hadi Desemba 2025, zaidi ya viti 700 vya kisasa vya matibabu ya kinywa na meno na mashine zaidi ya 600 za Periapical X-ray zilikuwa zimenunuliwa na kusambazwa nchini, sambamba na hospitali 27 za wilaya zikiwa zimenunua mashine za 2D OPG, huku hospitali 16 za Rufaa za Mikoa zikiwa na vifaa vya 3D CBCT, kwa kipindi cha Januari hadi Septemba 2026.
Dkt. Mfaume amewataka viongozi na wataalamu wanapaswa kuhakikisha vifaa hivyo vinatunzwa, vinahudumiwa kwa wakati na kutumika ipasavyo akielekeza mahitaji ya vyumba na vifaa vya radiolojia kuzingatiwa mapema wakati wa usanifu wa majengo.
Kuhusu rasilimali watu, Dkt. Mfaume amesema wataalamu 64 wa afya ya kinywa na meno wameajiriwa kwa kipindi cha Novemba 2025 hadi Oktoba 2026. Kati yao, 14 ni Madaktari wa Upasuaji wa Kinywa na Meno (DDS), 45 ni Matabibu wa Kinywa na Meno (DT) na watano ni Wataalamu wa Maabara ya Kinywa na Meno (DLT).
Dkt. Mfaume amehimiza Wizara ya Afya, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, halmashauri, taasisi za mafunzo, Chama cha Wataalamu wa Afya ya Kinywa na Meno Tanzania (TDA) na wadau wengine kushirikiana kutekeleza Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Afya ya Kinywa na Meno wa 2026–2031.