HUDUMA YA MADAKTARI BINGWA YARAHISISHA WANANCHI KUPATA MATIBABU YA KIBINGWA MBEYA
Posted on: September 20th, 2025
NA WAF - MBEYA
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mbeya, Dkt. Bwire Mbango, amesema huduma ya Madaktari Bingwa imekuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi kwani imerahisisha upatikanaji wa huduma za kibingwa na bobezi katika ngazi ya msingi, jambo linalopunguza usumbufu wa wananchi kusafiri mbali kufuata matibabu hayo.
Dkt, Mbango amesema hayo leo Septemba 19, 2025 mkoani Mbeya katika kambi ya Madaktari Bingwa wa Rais Samia kwenye hospitali ya Wilaya ya Mbeya.
Dkt. Mbango amesema ujio wa Madaktari Bingwa hospitalini hapo umewasaidia kuongeza uwezo kwa watumishi wote pamoja na Madaktari ambao wapo hospitalini hapo ili waweze kuboresha huduma zao na kuzitoa kwa kiwango cha ubora wa hali ya juu zaidi.
"Tumepokea Madaktari bingwa, kiujumla tumefurahi kwasababu wametusaidia kutuongezea uwezo kwa watumishi wetu wote pamoja na Madaktari ili waweze kuboresha huduma zao na kuzitoa kwa kiwango cha ubora wa hali ya juu zaidi," amesema Dkt. Mbango.
Aidha, Dkt. Mbango amesema ujio wa Madaktari Bingwa wa Dkt.Samia hospitalini hapo umeepelekea mapato kuongezeka kulinganisha na awali hii ni kutokana na idadi kubwa ya wananchi kujitokeza kwaajili ya kupata matibabu ya kibingwa.
"Ujio huu wa Madaktari Bingwa kwa siku zote ambazo wako hospitalini hapa, umechochea wananchi kujitokeza kwa wingi hivyo imetusaidia katika kuongeza mapato ya ndani ya hospitali hivyo tunatamani kampeni hii iongezewe wigo mpana na iwe endelevu" amesmea Dkt. Mbango
Kwa upande wake Daktari bingwa wa Usingizi na Ganzi salama, Dkt. Allen Kitalu amesema kufika kwao Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia imekuwa neema kubwa wameweza kusaidia kufunga mashine ya usingizi ambayo ilikuwa haitumiki tangu imepelekwe hospitalini hapo, lakini sasa mashine hiyo ya kisasa ya usingizi imeanza rasmi kutumika.