HUDUMA TABIBU ZA KIFAMASIA KUIMARISHWA KATIKA HOSPITALI ZOTE NCHINI
Posted on: September 26th, 2025
Na Waf, Dar es Salaam
Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea kuimarisha huduma zinazotolewa na mtaalam wa famasia mwenye ujuzi wa dawa za binadamu hospitali zote nchini ili kuhakikisha mgonjwa anapata dawa sahihi, kwa kipimo sahihi na kwa muda sahihi kulingana na hali yake ya kiafya.
Hayo yamebainishwa leo Septemba 25, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mifupa na Ubongo(MOI) Dkt. Mpoki Ulisubisya akimuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe katika maadhimisho ya siku ya Mfamasia Duniani ambayo Kitaifa yameadhimishwa Jijini Dar es Salaam.
Dkt. Ulisubisya amesema Ili kuzingatia umuhimu wa wafamasia katika kutoa huduma kwa wagonjwa Wizara ya Afya imeelekeza kuimarishwa kwa huduma za tabibu kifamasia katika hospitali zote za Rufaa za mikoa, kanda, Maalum na Taifa nchini.
"Nawapongeza sana viongozi na wafamasia wote katika hospitali ambazo zimekwishaanza na zinaendelea utekelezaji wa huduma hizo na wengine waige katika vituo hivyo ili vituo vyota viwe na watu wa kada hiyo itakayochangia ufanisi katika utoaji wa huduma za afya," amesema Dkt. Ulisubisya.
Naye Msajili wa Baraza la Famasi Tanzania Bw. Boniface Magige ametoa wito kwa wafamasia wote nchini kujitokeza kwa wingi kuongeza elimu ndani na nje ya nchi ili kuongeza wigo wa kutoa huduma hizo katika nyanja mbalimbali nchini.
"Takwimu za leo zinaonesha wafamasia nchini wamefikia 4,123 na wengine wanaendelea na mafunzo ya watarajali sehemu mbalimbali hivyo lazima tujipange kuongeza huduma katika jamii kwa kiwango na umahiri mkubwa," amesema Bw. Magige.
Kwa niaba ya Mfamasia Mkuu wa Serikali, Mfamasia kutoka Wizara ya Afya Bi. Aneth Wilboroad ameupongeza uongozi wa tume ya kikristo ya huduma za jamii (CCSC) kwa kushiriki kikamilifu katika kuadhimisha siku hiyo hapa nchini.
"Ni kweli kama wana taaluma Tulihitaji tukio kama hili la kukumbukwa ili kuadhimisha siku yetu ya wafamasia Duniani," amesema Bi. Wilbroad.