HOSPITALI YA WILAYA HANDENI YAPOKEA WAJAWAZITO 900 NDANI YA MIAKA MITATU
Posted on: February 24th, 2025
Na WAF - Handeni, Tanga
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga hadi sasa imeshapokea wajawazito 900 na kati yao 300 walijifungua kwa njia ya upasuaji ndani ya miaka mitatu(3).
Dkt. Samia ameyasema hayo leo Februari 23, 2025 alipokuwa akihutubia wananchi wa Handeni katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi ya Mkata, wilayani Handeni baada ya kuweka jiwe la msingi na kuizindua rasmi hospitali hiyo.
"Hospitali hii, viwango vyake ni vya kuwa hospitali ya mkoa na sio wilaya, kwani viwango vyake ni vya mkoa kwakuwa inatoa huduma zote kubwa muhimu," amesema Rais Samia.
Amesema, kusingekuwa na hospitali hiyo wajawazito hao 300 waliojifungua kwa njia ya upasuaji endapo wangekimbizwa Hospitali ya Tanga mjini au nyingine sio wote ambao wangefanikiwa kufika hospitali, kwani wengine wangefariki Dunia wakiwa njiani, hivyo imeokoa maisha ya wengi.
Rais Samia amefanya uzinduzi wa hospitali hiyo akiwa katika ziara mkoani Tanga ambayo ameanza leo Februari 23, 2025 hadi Machi 1, 2025 kwa lengo la kukagua na kuzindua miradi mbaliambali iliyotolewa fedha na Serikali.