Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

HOSPITALI YA RUFAA YA KANDA MBEYA YATOA ELIMU YA MAGONJWA MBALIMBALI NA UPIMAJI WA AFYA KWA WATU WENYE ULEMAVU 110 MKOA WA MBEYA

Posted on: April 7th, 2023

Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya leo imetoa mafunzo ya elimu ya afya ya magonjwa mbalimbali yakiwemo magonjwa yasioambukiza, afya ya akili, elimu ya afya ya uzazi na ujasiriliamali kwa walemavu zaidi ya 100 wa mkoa wa Mbeya lengo likiwa ni kuwawezesha kujua tabia zinazofanya mtu kuwa na afya nzuri na kuwakinga na maradhi mbalimbali.

Akizungumza mara baada ya kufungua mafunzo hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali Dkt. Godlove Mbwanji amesema kuwa, kundi la watu wenye ulemavu mara nyingi limekua ni rahisi kusahaulika hivyo kama hospitali imeandaa mafunzo hayo ili kuawezesha kujiamini na kuona wao ni sehemu ya jamii katika kufanya mambo makubwa ikiwa ni Jitihada za Serikali katika kutoa usaidizi wa kila namna kuhakikisha ustawi wa kila mmoja unazingatiwa.

“Hizi zote ni jitihada za Serikali inayoongozwa na Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Sulumu Hassan katika kuthamini watu wenye ulemavu na kuhakikisha kwamba watu wenye ulemavu nchi nzima wanathaminiwa, wapewa matibabu, wanapewa elimu ili waweze kujikinga na magonjwa.” - DKt. Mbwanji
Aidha Dkt. Mbwanji ametoa wito kwa Viongozi katika huduma za kijamii nchi kuendelea kuona namna ya kuwasaidia watu wenye ulemavu ili na wao waone ni sehemu muhimu ya jamii vilevile washiriki kikamilifu katika kukuza uchumi wa nchi ya Tanzania.

Naye Damasi Mwambeje Mwenyekiti wa Shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu mkoa wa Mbeya amemshukuru Serikali kwa kuwezesha kupatiwa mafunzo elimu ya afya na magonjwa mbalimbali pamoja na somo la ujasiriliamali yaliyoratibiwa na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya kwani kwa muda mrefu elimu hiyo haijawafikia wao kama watu wenye ulemavu kutokana na fikra potofu zilizoko kwenye jamii.

Zaidi ya washiriki 110 wenye ulemavu wamepataiwa mafunzo ya elimu ya magonjwa mbalimbali, Elimu ya Afya ya Akili, Ujasiriamali pamoja na kuchunguza afya bila malipo.