Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

HOSPITALI YA NYASA KUANZA KUTOA HUDUMA YA KINYWA NA MENO

Posted on: October 31st, 2024

Na WAF - NYASA

Timu ya Madaktari Bingwa wa Rais Samia iliyoweka kambi wilayani Nyasa mkoani Ruvuma imefanikiwa kuzindua huduma mpya ya kinywa na meno katika Hospitali ya wilaya ikiwa ni muendelezo wa kambi ya kibingwa awamu ya pili Wilayani humo.

Akizungumza Hospitalini hapo Daktari bingwa wa kinywa na meno Dkt. Luciana Albert kutoka hospitali ya Taifa Muhimbili amesema uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali hasa kwenye vifaa tiba umefanikisha hilo na sasa wananchi watapata huduma zote za kinywa na meno katika Hospitali ya wilaya ya Nyasa na kupunguza adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hiyo.

"Kuwa na vifaa ni jambo moja lakini kutumika ni jambo lingine, tumefika na kukuta tayari serikali imesha leta kiti kipya na cha kisasa kwa ajili ya matibabu ya kinywa na meno ambacho kina kila kitu kinachohitajika kwa ajili ya matibabu ya kinywa na meno. Tutaanza kutumia kwani kuna taratibu chache zimebakia kukikamilisha ili kiweze kufanya kazi kwa uwezo wake wote,” amesema Dkt. Albert.

Dkt. Albert amesema huduma hiyo ya kinywa na meno ipo sio kwaajili ya kutoa meno tu kwani kuna kasumba ya kuwa kila anayefika Hospitalini kwa sababu ya matatizo ya meno ni lazima atolewe jino, na kuwasihi wananchi kufika Hospitalini kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kinywa na meno sio mpaka mtu afikie hatua mbaya.

“Mtu asihangaike kwenda kwa watu wasio wataalam kwa sababu ya jino, anaweza kwenda huko akatolewa jino ambalo halikuhitaji hata kutolewa na akapata madhara, sasa huduma hii ipo hapa na kuna kifaa cha kisasa kabisa cha matibabu ya kinywa na meno, hivyo wananchi msisubiri hadi mkose usingizi kwa sababu ya maumivu ya jino ndipo muanze kutafuta huduma. Fika katika Hospitali hii ya wilaya ya Nyasa hata kwa uchunguzi tu,” amesema Dkt. Albert.

Bw. Chriss Mwafongo fundi sanifu wa vifaa tiba katika Hospitali ya wilaya ya Nyasa ameishukuru serikali kwa uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya Afya kwani zamani ilikuwa ni vigumu kupata kitanda cha kisasa kwa ajili ya matibabu ya kinywa na meno katika ngazi ya Afya ya msingi.