Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

HANANG CHUKUENI TAHADHARI DHIDI YA MAGONJWA YA MLIPUKO-DKT. SAMIA.

Posted on: December 7th, 2023

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa wananchi Mji mdogo wa Katesh Wilaya ya Hanang Mkoani Manyara na Watanzania kwa ujumla kuendelea kuchukua tahadhari za magonjwa ya mlipuko kwa kuchukua hatua za matumizi ya maji safi na salama.

Dkt. Samia ametoa wito huo leo Disemba 7 ,2023 wakati akizungumza na wananchi  mji mdogo wa Katesh Wilayani Hanang Mkoa Manyara baada ya Disemba 3, 2023 kukumbwa na maafa ya mafuriko yaliyosababisha maporomoko ya udongo kutoka mlima Katesh na kusababisha madhara makubwa ikiwemo majeruhi,vifo na upotevu wa mali.

"Jambo kama hili linapotokea huwa yanatokea magonjwa ya mlipuko ,niwaombe wananchi wachukue hatua stahiki za kuzingatia kanuni za afya pindi wanapotumia maji wazingatie kuepuka magonjwa ya mlipuko ikiwemo kuhara "amesema.

Aidha, Rais Samia ametoa maagizo kwa Wizara ya Afya kuhakikisha elimu na ufuatiliaji kwa kina inatolewa kwa wananchi.

"Wizara ya Afya hakikisheni elimu juu ya kujikinga na madhara yanayoweza kutokea kutokana na mafuriko inatolewa pia kufuatilia kwa kina majeruhi mpaka kuhakikisha wanakuwa katika hali ya kawaida"amesema Dkt Samia.

Halikadhalika, Dkt.Samia ameagiza kuhakikisha msaada wa Kisaikolojia unaendelea kutolewa pamoja na huduma za maji safi na salama kuendelea kuimarishwa.

Hata hivyo,ametumia fursa hiyo kuwashukuru wadau kwa kutoa msaada ambapo jumla ya Tsh.Bilioni 2.5 zimetolewa na wadau kutoka nje ya nchi huku akielekeza zitumike kujenga makazi ya kudumu kwa waathiriwa.