Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

HAMASISHENI WANANCHI KUZIBA MENO SIO KUNG’OA

Posted on: October 31st, 2024

Na WAF - Njombe

Wito umetolewa kwa Madaktari Viongozi wa Kinywa na Meno kwa ngazi za Mikoa, Halmashauri, Hospitali za Mikoa, kanda na Taifa kuhamasisha wananchi kuziba meno badala ya kung’oa kwa kuwa Serikali imeweka miundombinu rafiki na ya kuridhisha katika utoaji wa huduma hizo.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba, Wizara ya Afya, Dkt. Hamad Nyembea Oktoba 29, 2024 wakati wa Mkutano wa Mwaka wa Madaktari Viongozi wa Kinywa na Meno wa mkoa, unaoendelea mkoani Njombe kwa siku mbili kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Mji Njombe.

“Nazipongeza Hospitali za Rufaa, Mikoa na Halmashauri kwa kusimamia kwa vitendo dhima ya “Dawa ya jino siyo kungoa” jino linatibika, hivyo Tanzania bila vibogoyo inawezekana,” amesema Dkt. Nyembea.

Amesema kuwa maboresho yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita kwenye matibabu ya kinywa na meno ni ya kihistoria na yameleta mapinduzi makubwa katika eneo hilo ambapo kuna ongezeko kubwa la watu wanaoziba meno kutoka asilimia 2 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 41 mwaka 2024.

Takwimu hizo zinaenda sambamba na ununuzi wa viti vya kisasa vya kinywa na meno (Complete Dental Chairs) vipatavyo 207 kuanzia Januari – Desemba 2023 kwa gharama ya fedha za kitanzania Shilingi Bilioni 4.3, ununuzi wa mashine za kidijitali za mionzi za meno 102, zenye thamani ya Shilingi Milioni 999.6 zimenunuliwa na kufungwa katika Hospitali za Taifa, Kanda, Rufaa, Mikoa, Halmashauri na vituo vya Afya nchini.

Dk. Nyembea ametumia jukwaa hilo kuagiza usitishaji wa matumizi ya dawa ya kuziba meno aina ya AMALGAM kutokana na madhara yake kwa binadamu na uchafuzi wa mazingira kutokana na kiambata hicho, na badala yake akaagiza waganga wakuu wa mikoa, wilaya, waganga wafawidhi wa hospitali za rufaa za mikoa, kanda na maalumu, kuhakikisha wanatumia dawa aina ya CENTION kwa matibabu hayo ya kuziba jino.