Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

HAKUNA HOSPITALI YA WILAYA ITAACHWA NA MADAKTARI BINGWA WA RAIS SAMIA KWA SABABU YA JIOGRAPHIA

Posted on: June 2nd, 2024



Na WAF -Pwani

Mapema leo Juni 2, 2024 Jumapili saa kumi na moja jioni Madaktari Bingwa wa Rais Samia wameondoka uwanja wa Kimataifa wa Mwl. Nyerere Jijini Dar Es Salaam kuelekea kisiwa cha Mafia kwa ajili ya kutoa huduma za kibingwa katika hospitali ya wilaya ya Mafia, pamoja na ukweli kwamba geographia ya wilaya ya mafia ilivyo bado Madaktari Bingwa wa Rais Samia wanachanja mbuga kila mahali.

Madaktari Bingwa watano waliosafiri leo kuelekea kisiwa cha Mafia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya ndani, Daktari Bingwa wa magonjwa ya akina mama na uzazi, Daktari Bingwa wa ganzi na usingizi, Daktari Bingwa wa upasuaji na Daktari Bingwa wa magonjwa ya watoto.

Aidha, Madaktari Bingwa hawa wa Rais Samia wataweka kambi ya siku tano kuanzia kesho tarehe 03 Juni, 2024 hadi Ijumaa ya tarehe 07 Juni, 2024.

Lengo la kambi hizi ni kuwasogezea wananchi Huduma za kibingwa karibu ili kuwapunguzia gharama wananchi kufuata huduma hizi mbali.

Pia, kiongozi wa Madaktari Bingwa walioelekea Kisiwani Mafia Dkt. Mwasamila amesema pamoja na kwamba kambi hii ya madaktari Bingwa ni kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi pia itatoa nafasi kwa madaktari kujifunza na kubadilishana uzoefu katika mazingira tofauti ya kazi kwa watoa huduma na madaktari waliopo katika Hospitali ya wilaya ya Mafia.