HAKIKISHENI WANANCHI WANATUMIA MAJI SAFI NA SALAMA ILI KUJIKINGA NA MAGONJWA YA KUAMBUKIZA
Posted on: November 3rd, 2024
Na WAF - Simiyu
Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu amewataka wataalamu wa afya na uongozi wa mkoa wa Simiyu kuhakikisha kuwa wananchi wa mkoa huo wanatumia maji safi na salama katika maeneo yote ili kujikinga dhidi ya magonjwa ya kuambukiza hasa ugonjwa wa kipindupindu.
Prof. Nagu amesema hayo Novemba 2, 2024 katika ziara yake mkoani humo, yenye lengo la kufanya usimamizi shirikishi na kuangalia utekelezaji wa masuala mbalimbali ya sekta ya afya ikiwemo utayari na namna ambavyo wanakabiliana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo ugonjwa wa kipindupindu.
"Katika kipindi hiki cha mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu ni lazima tutumie mbinu zote kusitisha mnyororo wa maambukizi ya vimelea vinavyosababisha kipindupindu. Tufanye jitihada zote ili maji yapatikane bila kizuizi cha fedha kwa maeneo yenye miradi ya maji; na kwa yale maeneo ambayo hakuna miradi ya maji tupeleke maji. Aidha, kwa hatua za haraka visima vifupi viwekewe mazingira ya salama zaidi kwa kuvifunika na kuweka pampu za mikono," amesema Prof. Nagu.
Aidha, Mganga Mkuu amesisitiza umuhimu wa kutoa elimu kwa wananchi ili waone umuhimu wa kuzingatia kanuni za afya, hasa kujenga na matumizi sahihi ya vyoo bora sambamba na kunawa mikono baada ya kutoka maliwatoni.
Prof. Nagu amewataka wataalamu hao kufanya uchambuzi wa kina juu ya hali ya upatikanaji wa maji safi na salama katika mkoa huo kwa kukaa pamoja kuangalia kwa ufasaha hali ya upatikanaji wa maji na usalama wake kisha kuja na suluhu ili wananchi wawe salama.
Pia Prof. Nagu ameutaka uongozi wa mkoa huo kuhakikisha afua za unawaji mikono zinaimarishwa kwa kuweka miundombinu ya maji tiririka ya kunawa mikono katika maeneo mbalimbali yenye mikusanyiko.
"Niombe sana watendaji wahusishwe kuhakikisha kwamba kwenye maeneo yao kuna miundombinu ya vyoo bora pamoja na sehemu za maji tiririka ya kunawia mikono," amesema Prof. Nagu.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa huo Bw. Juma Topera ameishukuru Serikali na wadau wa sekta ya afya kwa kuendelea kuwashika mkono kupambana na magonjwa ya mlipuko na ya kuambukiza mkoani humo.