Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

HAKIKISHENI KILA MTAA, KIJIJI KUNA KIKUNDI CHA MAZOEZI

Posted on: November 17th, 2024

Na WAF - Dodoma

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ameelekeza wakuu wa wilaya na watendaji wa mitaa na vijiji katika mkoa huo kuhakikisha kila mtaa unakuwa na kikundi cha kufanya mazoezi (Jogging Club) ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.

Mhe. Senyamule ametoa maelekezo hayo Novemba 16, 2024 katika mazoezi ya Jogging ya pamoja mkoani Dodoma yenye lengo la kuhamasisha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na watu kufanya mazoezi ili kuepukana na tabia bwete.

“Nitoe maelekezo kwa wawakilishi wa wakuu wa wilaya tuhakikishe kila mtaa ama kijiji katika mkoa wetu wa Dodoma tuanzishe suala la Jogging Club iwe ya kukimbia ama kutembea ili kujenga msingi wa kufanya mazoezi katika mitaa yetu na wananchi wetu kuwa na afya bora,” amesema Mhe. Senyamule.

Mhe. Senyamule amesema kupitia mazoezi hayo Wizara ya Afya imetukumbusha kuhakikisha kuwa na moyo thabiti na dhamira ya kweli na kujipenda na kujithamini kwa kuchukua hatua ya kufanya mazoezi ambayo yatapunguza vifo kwa asilimia 33 ambavyo vinatokana na magonjwa yasiyoambukiza.

“Mazoezi haya tunapofanya katika mitaa yetu yatatumika pia kuzungumzia juu ya amani ya mtaa wenu, masuala ya maendeleo juu ya afya zetu na vitu vingine ambavyo tukivifanya kwa moyo mmoja vitasaidia Dodoma na Tanzania kiujumla kuwa na watu wenye afya bora,” amesema Mhe. Senyamule.

Pia Mhe. Senyamule amewasihi wananchi wa mkoani humo kutumia fursa ya uchunguzi na upimaji wa magonjwa unaoendelea katika viwanja vya Nyerere square kufika maeneo hayo ili kujua hali za afya zao.

“Tumeambiwa pale Nyerere Square wapo wenzetu wa Wizara ya Afya wanatoa huduma mbalimbali za kupima afya, utoaji damu na vitu vingine, hiyo ni fursa kubwa twendeni tukaungane nao kwa kupima afya zetu na huduma mbalimbali zinazoendelea katika eneo lile,” amesema Mhe. Senyamule.