HAKIKISHENI HUDUMA ZA MATIBABU YA KIBINGWA ZINAWAFIKIA WANANCHI WA HALI YA CHINI
Posted on: August 15th, 2024
Na WAF – Dar es Salaam
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amewataka wafanyakazi wa wizara hiyo kuhakikisha huduma za kibingwa za matibabu ya magonjwa mbalimbali zinawafikia wananchi wa hali ya chini bila ya kuwa na vikwazo vyovyote.
Waziri Mhagama ametoa kauli hiyo leo Agost 15, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na Manejimenti na watumishi wa wizara hiyo katika ofisi ndogo za wizara ya Afya mara baada ya kuapishwa ikulu mchana wa leo.
Waziri Mhagama amesema Serikali imefanya uwekezaji mkubwa wa vifaa tiba vya kisasa, kujenga majengo ya kisasa, kusomesha wataalamu na kuboresha maslahi ya wafanyakazi jukumu lililobaki kwao ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za matibabu.
“Kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali yetu asilimia 95 ya huduma za matibabu ya kibingwa zinapatikana hapa nchini ni jukumu lenu kuhakikisha uwekezaji huu uliofanywa na Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan unawafikia wananchi wengi zaidi waliopo ndani na nje ya nchi yetu”Amesema Waziri Mhagama.
Pia amesisitiza watoa huduma za afya kuendeleza matumizi bora ya lugha za staha na kuimarisha mawasiliano na wagonjwa katika maeneo yao ya kutolea huduma.
“Kuna wakati mgonjwa anahitaji kupata maneno mazuri ya faraja na akipata mane no hayo kwa asilimia kubwa anakuwa na matumaini ya kupona ugonjwa wake, tunahitaji kuwasaidia watanzania kwani sisi tumebeba usalama wa afya za watanzani hivyo basi tutimize wajibu wetu wa kazi kwa kufuata sera na miongozo iliyopo”, Amesema Waziri Mhagama.
Akizungumzia kuhusu tiba utalii Mhe. Mhagama alisema miaka michache iliyopita hakukuwa na uwekezaji wa kutosha katika sekta ya afya kutokana na uwekezaji uliofanyika wananchi kutoka nchi za jirani wanakuja kutibiwa hapa nchini.
“Mimi na viongozi wenzangu tutatoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha wizara yetu inakwenda mbele zaidi na kutoa huduma bora kwa watanzania na wasio watanzania ambao wanakuja katika nchi yetu kupata huduma za matibabu”, Amesema Waziri Mhagama.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya Mhe. Godwin Mollel alimpongeza Waziri Mhagama kwa kuteuliwa kuwa waziri wa wizara hiyo na kusema kuwa uzoefu aliokuwa nao utasaidia kuifikisha wizara hiyo mbali Zaidi huku Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. John Jingu akisema kazi kubwa ya wizara ya Afya ni kuzuia magonjwa, kutibu na kupambana na magonjwa yanayoibuka pamoja na kutekeleza majukumu mengine yaliyopo ya kuhakikisha usalama wa afya unakuwepo nchini.