GEITA YALENGA KUONGEZA VITUO VINAVYOFIKIA NYOTA TATU KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA KWA WANANCHI
Posted on: October 26th, 2026Na Amos Luzuga, WAF-GEITA
Wizara ya Afya imefanya tathmini ya ubora katika vituo sita vya kutolea huduma za afya ya msingi mkoani Geita, Oktoba 26, 2026, kwa lengo la kubaini maboresho katika rasilimali watu, vifaa tiba, miundombinu na utoaji wa huduma, hatua inayolenga kusaidia Mkoa huo kufikia lengo la angalau asilimia 80 ya vituo hivyo kuwa na nyota tatu au zaidi.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Afisa Ubora kutoka Wizara ya Afya ambaye pia ni Mratibu wa zoezi hilo la tathmini kitaifa Bw. Erick Kinyenje, amesema tathmini hiyo inapima hali ya vituo katika maeneo mbalimbali yanayoathiri ubora wa huduma.
“Katika zoezi hili tunaangalia ubora wa vituo katika maeneo yote, ikiwemo uwepo wa watumishi, vifaa tiba, majengo na huduma zinazotolewa kwa ujumla,” amesema Bw. Kinyenje.
Vile vile Bw. Erick amesisitiza kuwa zoezi hilo linatarajia kufikia vituo zaidi ya Elfu tatu nchini na matokeo ya tathmini itakayopatikana itaweza kusaidia kubaini mahitaji ya kila kituo na kuelekeza hatua za kuboresha maeneo ambayo hayajakidhi viwango vinavyotakiwa.
Aidha Bw. Kinyenje ameeleza kuwa tathmini hiyo ni endelevu na ilianza mwaka 2015, huku Wizara ya afya ikiendelea kutoa elimu kwa viongozi wa sekta ya afya kuhusu umuhimu wa viwango vya ubora.
Hata hivyo amesema kuwa matokeo hayo pia yanaweza kusaidia kupanga mahitaji ya watumishi na rasilimali nyingine, pamoja na kuboresha uwezo wa vituo katika kutoa huduma kwa ufanisi zaidi.
Katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora viongozi wa vituo wamesisitizwa pia umuhimu wa kutumia matokeo ya tathmini kuweka vipaumbele, kurekebisha mapungufu yaliyobainika na kufuatilia utekelezaji wa maboresho, ili kuongeza idadi ya vituo vinavyofikia nyota tatu au zaidi na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, salama na zinazokidhi mahitaji yao.