FANYENI KAZI KWA WELEDI KUJENGA TASWIRA YA SERIKALI
Posted on: March 14th, 2025
NA WAF - MWANZA
Watumishi wa Wizara ya Afya wamehimizwa kufanya kazi kwa weledi, maarifa na maelewano nbaina yao katika kuwahudumia wananchi ili kujenga taswira njema ya Serikali.
Rai hiyo imetolewa Machi 13, 2025 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekhalaghe wakati akifunga kikao cha baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Afya lililofanyika mkoani Mwanza.
Dkt. Shekalage amebainisha kuwa ni muhimu kutambua kuwa wajibu wetu ni kutoa huduma, hivyo kila mmoja afanye kazi kwa weledi na kwamba haki inakuja baada ya kuwajibika.
Dkt. Shekalage amesema uwekezaji mkubwa umefanywa katika sekta ya afya ambao ni pamoja na miundombinu vifaa na kusomesha wataalam, hivyo kilichobaki ni kuimarisha huduma kwa kuwajali wateja wakati wote.
"Suala la huduma kwa wateja lifanyiwe kazi, watumishi wa afya wafundishwe kila wanapoanza kazi na iwe zoezi endelevu," amesisitiza Dkt. Shekalage.
Dkt. Shekalage amewahimiza watumishi kupendana wao kwa wao na kushirikiana katika kutatua changamoto zinazojitokeza sekta ya afya na kujiepusha na migogoro wakitambua wanajenga nyumba moja.
Amebainisha kuwa migogoro kazini hupunguza ufanisi na kuchangia kudhoofisha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.
Pia, amewataka viongozi wa ngazi mbalimbali kuwapatia ujuzi wa uongozi ikiwa ni pamoja na kujifunza kutoka kwa wengine wanaofanya vizuri ili kuleta tija kwenye utendaji kazi.
Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Afya limekuwa na kikao chake cha siku mbili jijini mwanza ambapo pamoja na mambo mengine wajumbe hao wamepitia mpango wa bajeti wa mwaka 2025/26 utakaotekeleza shughuli za sekta ya Afya.