Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

FANYA MAZOEZI, EPUKA MWILI ZEMBE

Posted on: October 15th, 2024

Na WAF - Mwanza

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewahimiza wananchi kufanya mazoezi ili kuepuka tabia bwete inayosababisha kupata magonjwa yasiyoambukiza.

Rais Dkt. Samia amesema hayo leo Oktoba 14, 2024 kwenye kilele cha maadhimisho ya Mbio za Mwenge wa Uhuru, katika uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza, ambayo yamewakutanisha viongozi mbalimbali wa nchi akiwemo Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango.

"Niwahimize sana, suala la michezo na mazoezi kwa vijana, ili kujikinga dhidi ya na maradhi ya shinikizo la juu la damu (Presha), kisukari, pamoja na masuala ya saratani ambayo yanatokana na mwili zembe," amesema Rais Dkt. Samia

Aidha, Rais Samia amesema, kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya, kuongezeka kwa kasi kwa magonjwa yasiyoambukiza kunatokana na mtindo wa maisha na kutofanya mazoezi.

"Wanangu, watoto wangu, vijana wangu, mazoezi ni kitu cha muhimu, michezo ni jambo la muhimu sana," amesisitiza Rais Dkt. Samia