ELIMISHENI WANANCHI UMUHIMU WA BIMA YA AFYA KWA WOTE- MAJALIWA
Posted on: October 31st, 2024Na WAF, Arusha
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Afya kuandaa mkakati mzuri wa kuelimisha wananchi juu utekelezaji wa Bima ya Afya kwa wote.
Mhe. Majaliwa ametoa agizo hilo leo Oktoba 30, 2024 wakati akimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa kongamano la Bima ya Afya kwa Wote na Jukwaa la Kitaifa la Ugharamiaji wa Huduma za Afya kwa ajili ya utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote (Universal Health Insurance - UHI).
Mhe. Majaliwa amesema utoaji wa elimu kwa jamii ni muhimu ukapewa kipaumbele ili kuhamasisha wananchi wengi kujisajili na kunufaika na huduma bora ya afya kwani Serikali imewekeza miundombinu ya kutosha ya vifaa tiba pamoja na ujuzi wa madaktari kuanzia ngazi ya zahanati hadi taifa.
Amesema pia ili kufanikisha mpango huu wadau wanapaswa kushirikishwa kwa karibu pamoja na kuhakikisha kuwa kunakuwa na vyanzo endelevu vya mapato na kuwa na mfumo wa uchagiaji ambao hautaumiza wananchi.
"Serikali imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni 173 katika mwaka wa fedha 2024/25 kwa ajili ya mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote, lakini fedha hizi hazitatosheleza mahitaji ya Watanzania wote wasio na uwezo, hivyo mnapaswa kubuni vyanzo vya mapato endelevu," amefafanua Mhe. Majaliwa.
Kongamano hilo linalofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Arusha, limelenga kuwashirikisha wadau wote muhimu kuweka mikakati madhubuti ya utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote.
Kaulimbiu ya Kongamano hilo ni; Ugharimiaji end elevu wa huduma za afya nchini: Kuimarisha mfumo wa Bima ya Afya ili kufikia afya kwa wote 2030.