Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

EBOLA: ZAIDI YA WAANDISHI WA VYOMBO VYA HABARI 30 WAPATIWA MAFUNZO KAGERA

Posted on: October 5th, 2022

Na. Hassan Kimweri, WAF - Kagera

Waandishi wa Habari mkoani Kagera wameshauriwa kutoa taarifa sahihi juu ya ugonjwa wa Ebola ambao umekuwa tishio na kuuwa watu nchini Uganda.

Kauli hiyo imetolewa leo na Afisa Habari Mwandamizi kutoka Wizara ya Afya Bw. Said Makora alipokua anatoa mafunzo kwa waandishi wa Habari wa Mkoa huo juu ya namna bora ya kutoa taarifa za Ebola kwa wananchi.

"Mnatakiwa mfanye vipindi vinavyoelimisha jamii na kuwapa mbinu sahihi za kujikinga na ugonjwa huu wa Ebola maana Ebola ni hatari sana na njia za kujikinga ni kama zile za UVIKO-19 ikiwemo ya kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni mara kwa mara." Amesema Bw. Said

Akibainisha njia za kujikinga na ugonjwa huo Bw. Said amesema ni pamoja na kuepuka kugusa au kutumia vyombo, matandiko na nguo za mtu aliyehisiwa kuwa na dalili za ugonjwa wa Ebola na kuepuka kusalimiana kwa kushikana mikono au kukumbatiana.

Ugonjwa wa Ebola ni ugonjwa hatari sana unasababishwa na Virusi na ni miongoni mwa Magonjwa ya milipuko yajulikanayo kama Homa za Virusi yanayoweza kuambatana na kutokwa na damu mwilini.

"Dalili ya kutokwa na damu mwilini hutokea mara chache kwa baadhi ya wagonjwani hivyo tutoe elimu zaidi kwa wananchi kuwaambia kwa dalili nyingine kama Homa, kutapika, kuharisha, kuishiwa nguvu au kuumwa na kichwa watoe taarifa au kufika katika vituo vya kutolea huduma za Afya vilivyo karibu yao." Amesema Bw. Said

Mafunzo hayo yamehudhuriwa na waandishi wa vyombo vya Habari zaidi ya 30 ambayo yametolewa mkoani Kagera kwa lengo la kuwajengea uwezo waandishi wa habari kutoa elimu sahihi juu ya kukabiliana na Ebola endapo ugonjwa huo utaingia nchini.