DKT. SAMIZI ASISITIZA USHIRIKIANO KAZINI
Posted on: December 30th, 2025Na, WAF - Dar es Salaam
Wito umetolewa kwa Watumishi wa Sekta ya Afya kuhusu umuhimu wa kuwa na mshikamano, ushirikiano na uwajibikaji miongoni mwao katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Florence Samizi kwenye kikao maalum na watumishi wa Idara ya Kinga cha kupitia utekelezaji wa shughuli za kinga Desemba 30, 2025 katika Ofisi za ndogo ya Wizara ya Afya jijini Dar es Salaam.
Katika kikao hicho kilicholenga kujadili hali ya utekelezaji wa majukumu ya kinga, mafanikio yaliyopatikana pamoja na changamoto zinazojitokeza katika kudhibiti magonjwa na kulinda afya ya jamii, Dkt. Samizi amesisitiza umuhimu wa mshikamano, ushirikiano na uwajibikaji miongoni mwa watumishi katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku, akieleza kuwa huduma za kinga zina mchango mkubwa katika kuimarisha na kulinda afya ya Taifa.
“Idara ya Kinga ni mhimili muhimu wa sekta ya afya kwa kuwa inalenga kuzuia magonjwa kabla hayajatokea. Ushirikiano na uwajibikaji wenu ndiyo msingi wa mafanikio ya kazi hizi” amesema Dkt. Samizi.
Ameongeza kuwa watumishi wanapaswa kuendelea kuboresha mifumo ya kazi, kuimarisha matumizi ya takwimu sahihi pamoja na kuhakikisha taarifa zinawasilishwa kwa wakati ili kuwezesha Wizara kuchukua hatua za mapema katika kudhibiti changamoto za afya ya umma.
Kwa upande wao, watumishi wa Idara ya Kinga wamebainisha kuwa ushirikiano kati ya Sehemu na programu mbalimbali umechangia kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa shughuli za kinga katika maeneo tofauti nchini.
Maeneo yaliyopitiwa katika kikao hicho ni pamoja na utekelezaji wa programu za chanjo, ufuatiliaji wa magonjwa ya mlipuko, magonjwa yasiyopewa kipaumbele, afya ya mazingira pamoja na utayari na mwitikio wa dharura za afya ya umma.