Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

DKT. MPANGO AIASA JAMII KUACHA UNYANYAPAA KWA WAVIU

Posted on: December 2nd, 2024

Na WAF - Ruvuma

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Phillip Mpango ameitaka jamii kuondona na dhana potofu ya unyanyapaa kwa watu wenye virusi vya UKIMWI.

Dkt. Mpango ametoa rai hiyo leo Disemba 1, 2024 wakati akihitimisha maadhimisho ya wiki ya siku ya UKIMWI duniani ambayo kitaifa yamefanyika katika mji wa Songea Mkoani Ruvuma.

Dkt. Mpango amesema mtazamo hasi dhidi ya waathirika wa Virusi vya UKIMWI unachangia kwa kiasi kikubwa kurudisha nyuma jitihada za Serikali katika kukabiliana na mapambano dhidi ya UKIMWI nchini.

"Tatizo sugu la unyanyapaa na ubaguzi katika jamii ni jambo ambalo linasababisha WAVIU waonekane wametengwa hali inayosababisha watu wengi kuogopa kupima. Hali hii inarudisha nyuma jitihada za Serikali kukubaliana na maambukizi ya UKIMWI," amesema Dkt. Mpango.

Ameendelea kutoa rai kwa wananchi hususan wanaume kujitokeza kupima ili kujua hali zao za maambukizi na sio kutegemea majibu ya mke akipima na kukutwa yupo salama na yeye anaona yuko salama pia.

Aidha, Dkt. Mpango ameongeza kuwa Serikali inafanya jitihada za kuendelea kutoa elimu kwa mtu, familia na jamii kwa ujumla juu ya uelewa wa VVU na UKIMWI ili jamii iweze kuepukana na maambukizi mapya ambayo mengi uchangiwa na unywaji wa pombe uliopindukia, kuwa na wapenzi wengi na ngono zembe.

Hata hivyo, Makamu wa Rais huyo ametoa wito kwa kundi la vijana hasa wa kike ambao ndiyo wanaonekana kuwa katika hatari zaidi kuepukana na makundi na viashiria ambayo yanachochea maambukizi mapya na hivyo kufifisha juhudi za Serikali katika kukabiliana na VVU na UKIMWI.

Maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani yanaadhimishwa kila ifikapo tarehe 1 Disemba ya kila mwaka ambapo mwaka huu kitaifa yamefanyika katika mji wa Songea mkoani Ruvuma.