DKT . MOLLEL: WATUMISHI LONGIDO KUPATIWA NYUMBA
Posted on: June 23rd, 2024
Na WAF, Longido- Arusha
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel, ameziagiza Timu za Afya za mkoa na wilaya kutoa kipaumbele katika kuwapatia makaazi watumishi wa Wilaya ya Longido.
Dkt. Mollel amezitaka timu za uendeshaji wa huduma za afya (CHMT) wilayani Longido na RHMT Mkoa wa Arusha wakati wa ziara yake wilayani humo.
"Mhakikishe Zahanati ya kijiji cha Wosiwosi Kata ya Gelai Lumbwa wilaya ya Longido inapewa kipaumbele cha kupatiwa nyumba ya daktari ili kusaidia wakazi wa eneo hilo kuondokana na adha ya kutembea umbali wa mwendo mrefu kufuta Huduma za afya" amesema Dkt. Mollel na kuongeza
"Dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani ni kupunguza vifo vya mama na mtoto ndio maana amefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya kwa kuboresha miundombinu, kuongeza upatikanaji wa vifaa tiba”, ameeleza Dkt. Mollel.
Hivyo amesema CHMT na RHMT watakapo kuwa wanaandika mipango yao wahakikishe Zahanati ya Wosiwosi inapangiwa kupatiwa nyumba ya daktari wa kuhudumia wananchi wa kijiji cha Wosiwosi.
Aidha ameongeza kuwa katika maeneo ambayo yako pembezoni wanapoanza ujenzi wahakikishe wanaweka bajeti inayo jumuisha vitu vyote muhimu ikiwemo nyumba ya daktari.
Wakati huo huo, ameupongeza uongozi wa kata hiyo kwa kushirikiana na wananchi kuunga jitihada za Rais Samia kwa kuchangia kiasi cha Shilingi milioni nane kwa ajili ya ujenzi wa zahanati hiyo.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Longido ambaye pia ni Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa amesema Jimbo la Longido linamahitaji makubwa ya nyumba za madaktari hali ambayo inasababisha zahanati nyingi zilizokamilika kushindwa kutoa Huduma kwa wananchi.
Dkt. Kiruswa amemuomba Dkt. Mollel kwa niaba ya Wananchi wa Jimbo hilo kuwasaidia zahanati kupata nyumba za wataalam wa afya ili kutoa huduma kwa wananchi na kuepuka vifo vitokanavyo na uzazi hasa wakati wa wakina mama wanapokaribia kujifungua.
Dkt. Kiruswa ameeleza kuwa kutoka wilaya ya Longido hadi katika kata hiyo ni umbali wa kilomita 140, hivyo ni vigumu kwa wananchi kufika huduma.
Lakini pia ameishukuru Serikali kwa kutoa kibali cha kuanzisha shule pamoja na fedha kwa ajili ya miradi ya afya, elimu na maji ambayo itakwenda kumaliza mahitaji muhimu ya wananchi katika jimbo hilo.
Mwisho