Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

DKT. MOLLEL: SERIKALI ITAJENGA MAJENGO YA KISASA KATIKA HOSPITALI ZETU

Posted on: August 6th, 2024



Na WAF Iringa

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, amesema Serikali itaendelea kuboresha huduma za afya na rasilimali muhimu ili kuhakikisha huduma za afya zinaendelea kuboreka katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa na maeneo mengine nchini.

Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Afya na Masuala ya Ukimwi katika hospitali hiyo, leo Agosti 06, 2024 Dkt. Mollel amebainisha kuwa Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa kwenye sekta ya afya ili kuboresha huduma za afya kwa wananchi na jamii kwa ujumla.

"Tunaendelea na jitihada za kuhakikisha huduma za afya zinaimarishwa katika hospitali zetu zote nchini. Serikali itaendelea kutoa msaada na rasilimali muhimu ili kufanikisha lengo hili," amesema Dkt. Mollel.

Aidha, Dkt. Mollel ameeleza kuwa Serikali inaweka mikakati madhubuti ya kuboresha majengo ya hospitali na kujenga majengo ya kisasa yatakayokidhi mahitaji ya hospitali bila kuathiri maeneo ya pembeni.

"Tumejipanga kuboresha majengo na miundombinu ya hospitali zetu kwa kuhakikisha tunajenga majengo ya kisasa yatakayokidhi mahitaji ya huduma za afya bila kuathiri maeneo jirani," ameongeza Dkt. Mollel.

Kamati ya Kudumu ya Afya na Masuala ya Ukimwi, inayoongozwa na Kaimu Mwenyekiti Mheshimiwa Christina Msava, imeipongeza hospitali hiyo kwa jitihada kubwa za kuboresha huduma za afya na kutoa huduma bora wakati wote.